NA BALTAZAR MASHAKA, MAGU
MBUNGE wa Magu(CCM),Bonventure Kiswaga amesema serikali ya awamu ya sita imeipatia wilaya hiyo zaidi ya sh.bilioni 107.294 za miradi ujenzi wa miundombinu ya maji,barabara,madaraja na elimu.
Ametoa takwimu hizo kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kitumba,Igekemaja,Busekwa na Kanyama vya kata za Kisesa,Bujashi na Bujora,jana wakati akihutubia wananchi katika mikutano ya hadhara akihitimisha ziara ya kutembelea kijiji kwa kijiji.
Amesema wananchi wa Magu katika suala la maendeleo hawana deni na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,amewapatia fedha nyingi zaidi ya bilioni 107.294, kwa fedha hizo alizoleta apewe kura za heshima kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu,wamuonyeshe heshima hiyo na fadhila kwa miradi ya maendeleo.z
“Nitazungumzia yanayotuunganisha,Rais Dk.Samia ametupatia fedha nyingi za kujenga barabara kwa kiwango cha lami na madaraja,ametoa sh.bilioni 43 za kujenga daraja la Simiyu kwa njia mbili,daraja la Ng’haya/Sukuma ambalo limepoteza maisha ya watu wengi sh.bilioni 11.3 na daraja la mfano Ihushi sh.bilioni 13,”amesema Kiswaga.
Ameitaja miradi mingine ni ujenzi wa barabara za urefu wa km 10 kutoka Magu-Kwimba kwa kiwango cha lami sh. bilioni 14 na Airport hadi Nyangunge,urefu wa km 10 kwa gharama ya sh.bilioni 14 huku barabara ya Kona ya Kayenze ikitengewa sh.milioni 350.
“Msituhukumu kwa barabara za vitongoji na vijiji,watu wameongezeka na mvua kubwa zilizonyesha zimeharibu barabara nyingi na mahitaji ni makubwa kuliko uwezo,tatizo ni uwezo wa serikali inatafuta fedha zikipatikana tutatengeneza,nawasihi tuvumilieni tunakwenda pole pole,”amesema Kiswaga.
Ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita kwa kutambua umuhimu wa elimu imetoa sh.bilioni 4.1 za kujenga shule ya sekondari Ihushi (wasichana) ya mfano mkoani Mwanza,kidato cha kwanza hadi cha sita.
Mbunge huyo wa Magu amesema maboma yote yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi yakihusisha sekta ya elimu na afya, serikali inatafuta fedha za kuyakamilisha yaanze kutoa huduma kwa jamii.
Akizungumzia nishati ya umeme amesema serikali imetenga bajeti ya kufikisha nishati hiyo katika vitongoji 4,000 vyenye hadhi ya vijiji kote nchini na haiwezi kumaliza tatizo hilo kwa wakati mmoja,hivyo wilayani Magu vitongoji 15 vitanufaika.
“Nafahamu umuhimu wa umeme ni uchumi,ukiwa nao vitu vitafanyika na unaweza kutengeneza vitu na viwanda vidogo,hivyo endeleeni kutuamini,nafahamu pia madhara ya kukosa maji,tuna mpango wa kuchimba visima ili kupunguza adha hiyo kwa wananchi ingawa hayatakidhi mahitaji,mradi wa Bujora utamaliza kero hiyo,”amesema Kiswaga.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bujora,Salome Julius,amesema kupitia ziara za mbunge,serikali ya awamu ya sita imetatua kero na changamoto mbalimbali zikiwemo za barabara,shule na maji ambapo imekamilisha miradi ya sh. bilioni 4.6 huku mingine ya sh.bilioni 1.3 ikiendelea.
Kwa upande wa madiwani wa kata za Kisesa na Bujashi, Joseph Kabadi na Lucas Deleli,wamesema serikali imeleta fedha za maendeleo ya wananchi kwa mtiririko ambayo Chama Cha Mapinduzi iliingia mkataba nao wa kuyatekeleza,inadhirisha viongozi waliopo wanafaa. Wamesema wananchi wasipowapigia kura za ushindi (mbunge,madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa), watakuwa wafanya dhambi kubwa kwa sababu maendeleo yanayozungumzwa leo,wangekuwa walaji wa fedha badala ya kuzimamia yasingekuwepo.