Dar es Salaam. Matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wazima na watoto nchini yameongezeka, ripoti mpya inaeleza.
Kwa watu wazima makosa yaliyobainika katika ripoti hiyo ni pamoja na shambulio la kudhuru mwili, kujeruhi, lugha ya matusi na shambulio la aibu.
Upande wa watoto, ripoti hiyo imetaja matukio ya ubakaji, ulawiti, kutupa watoto, kutelekeza familia na ukeketaji.
Hayo yamo katika ripoti ya takwimu za uhalifu na usalama barabarani ya mwaka 2023, iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania.
Ripoti hiyo ya kuanzia Januari hadi Desemba 2023 tayari imechapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ikionyesha Januari hadi Desemba, 2023 waathirika 22,147 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wazima waliripotiwa, wanawake wakiwa ni 13,322 na wanaume 8,825.
Takwimu hizo kwa mwaka 2023 ni kubwa zaidi ikilinganishwa na waathirika 18,403 walioripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2022 ikiwa ni ni ongezeko la waathirika 3,744 sawa na asilimia 20.3.
Aina ya matukio yaliyobainishwa kupitia ripoti hiyo ni shambulio (6,413), shambulio la kudhuru mwili (5,246), kujeruhi (3,729), lugha ya matusi (3,506) na shambulio la aibu (988).
Maeneo yaliyobainika kuwa mwiba wa ukatili na unyanyasaji kwa watu wazima ni Temeke yenye waathirika 4,214, Arusha yapo matukio 3,476, Tanga (2,368), Kinondoni (2,361) na Ilala (1,921).
Hata hivyo ilibainika mikoa iliyokuwa na idadi ndogo ya waathirika ni Kusini Pemba na Rufiji yenye tukio moja kila mmoja, Kusini Unguja na Kaskazini Pemba matukio matatu kila moja na Mjini Magharibi (11).
Ripoti hiyo imeeleza kuwepo kwa ongezeko kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto kwenye jamii, ambapo matukio mengi yanatendeka ndani ya familia na jamii.
Matukio hayo yanayowakumba watoto ni ubakaji, ulawiti, kutupa watoto, kutelekeza familia na ukeketaji.
Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2023 waathirika 15,301 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, waliripotiwa ikilinganishwa na waathirika 12,163 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Idadi hiyo ni ongezeko la waathirika 3,138 sawa na asilimia 25.8.
Makosa yenye idadi kubwa ya waathirika ni ubakaji (8,185), ulawiti (2,382), mimba kwa wanafunzi (1,437), kumzorotesha mwanafunzi kimasomo (922) na shambulio la aibu (396),
Mikoa iliyobainika kuwa changamoto ni Arusha (1,089), Mororgoro (976), Tanga (884), Kinondoni (789) na Mjini Magharibi (788).
Pia mikoa yenye idadi ndogo ya waathirika wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni Kusini Pemba matukio 100, Kusini Unguja (102), Kaskazini Pemba (103), Tarime Rorya na Kaskazini Unguja (161 kila mmoja).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukatili na unyanyasaji umekuwa ukiongezeka kila siku na jamii inashindwa kutetea watoto.
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, limeendelea kuinua kiwango cha uelewa wa jamii na kuimarisha huduma ya madawati ya jinsia katika vituo vya polisi, ili kuhamasisha wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto,” imeandikwa ripoti hiyo.
Akizungumzia ripoti hiyo, mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo Bisimba amesema ongezeko la matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yametokana na ugumu wa maisha.
“Mambo yamekuwa magumu watu hawafikirii kama kawaida, jambo dogo linamfanya mtu atende tukio lisilostahili,” amesema.
Dk Bisimba aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), amesema tatizo lingine linalochochea hali hiyo, ni changamoto ya afya ya akili inayotokana na matazamio ya watu juu ya jambo fulani ambalo baadaye hulikosa.
Amesema suluhisho ni maboresho juu ya mfumo wa elimu kwani vijana wengi wanasoma na kurudi mitaani baada ya matarajio yao kufa, jambo linalowaingiza kwenye matukio hatarishi.
“Vijana wengi wamesoma, wazazi wao wamekopa hadi wamemaliza chuo wanarudi mitaani hakuna ajira. Si kwamba hakuna ajira zipo lakini umesomea uhandisi unakwenda kuendesha bajaji ni vitu visivyoendana kwahiyo hii inavuruga akili ya watu wengi, tunapaswa kuliangalia hili kwa umakini,” amesema.
Amesema ni muhimu kuangalia kwa karibu makuzi ya watoto na pale dosari zinapobainika, zianze kushughulikiwa kwa karibu zaidi.
Ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kushughulikia changamoto kwenye jamii kabla ya kuibua matatizo makubwa.
Hoja hizo zinaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya kijamii, Dk Aidan Msafiri akisema, matukio hayo yapo kutokana na kiwango cha huruma kushuka kwenye jamii.
“Huruma ya watu kwenye jamii imeshuka, sababu kubwa watu wamekata tamaa kutokana na maisha magumu, familia zimesambaratika,watu hawapati eneo la kueleza matatizo waliyonayo,”amesema.
Pia Dk Aidan amesema kuendelea kuongezeka kwa matukio ya ukatili pia kunachochewa na tarifa ambazo jamii imekuwa ikizipokea hasa kuanzia asubuhi hadi jioni lazima kuwe na ripoti ya watu kupigana au kutenda mauaji hivyo jamii huathirika kisaikolojia.
“Utasikia huyu kaiba, kalawiti, kabaka hii sumu inaingia kwenye vichwa vya watu kwenye jamii na kuichochea jamii kutenda ukatili.Hata kwenye mitandao ya kijamii ukiingia matukio hayo yanaripotiwa na wengi ni vijana sio wazee,”alisema.
Akitoa tathmini yake, Dk Msafiri amesema watu wanaofanya matukio ya ukatili hawakulelewa na wazazi wote na kama wamelelewa na wazazi wote, wazazi hao hawana uwezo wa kulea.
Tathmini ya kisaikolojia inatolewa na mtaalamu wa saikolojia, Ramadhan Masenga akisema, msongo wa mawazo ndio kichocheo kuongezeka kwa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wazima.
“Watu wana hisia walizoficha ambazo hawawezi kuzitoa,hisia hizo zinaweza kuwa zimesababishwa na wakuu wao wa kazi,watu ambao hawawezi kuwafikia sasa hisia hizo lazima zitoke na zinakuja kutokea sehemu ambayo mtu amemkwaza na mtu anayehisi anammudu,”amesema.
Mbali na hayo, Masenga amesema kutokana na upendo kwa watu kupungua na watu kuhamishia kwenye fedha, madaraka na mali ni ngumu kuwa na hofu ya Mungu na upendo.
“Ili kudhibiti matukio haya, ni muhimu kuwa na uhusiano mzuri na hakuna mbadala wa uwepo wa watu, watu wanamiliki nyumba na mali lakini wakumbuke kama wamezungukwa na watu ambao hawathamini namna walivyo, vitu hivyo vinapoteza thamani,”amesema.
Kuhusu ugumu wa maisha, amesema kila mtu kwenye jamii anapaswa kutambua hali aliyonayo si yake peke yake kwani wapo watu wengi wanapitia hali hiyo.
Masenga amesema ni hatari kwa mtu kuzibeba changamoto anazopitia kama ni zake binafsi, kwani hatari huonekana kwenye familia nzima.