Geita. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewatahadharisha wananchi wanaofika kwenye vituo vya kujiandikisha na kutoa taarifa za uongo ili wajiandikishe kwa mara ya pili kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria na adhabu yake ni kifungo kuanzia miezi sita jela hadi miaka miwili au kulipa faini kati ya Sh100,000 na Sh300,000.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, alibainisha hayo Julai 25, 2024 mjini Geita alipozungumzia mwenendo wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, mzunguko wa kwanza, kwenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.
Jaji Mwambegele amesema kujiandikisha kuwa mpigakura zaidi ya mara moja ni kosa kisheria chini ya kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, namba 1 ya mwaka 2024.
Mwenyekiti huyo amesema yapo maneno ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya vyama vya siasa, kwamba mfumo wa uandikishaji unaruhusu kujiandikisha zaidi ya mara moja, jambo ambalo amesema si la kweli.
Amesema hoja hiyo imetokana na mpigakura, Andrew Kiyungi, mwenye kadi namba T-1003-3617-715-9, yenye jina la Tume ya Uchaguzi na kadi nyingine yenye namba hiyohiyo ikiwa na jina la Tume Huru ya Uchaguzi.
“Mtu huyu taarifa zake zinaonyesha amejiandikisha kwenye kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Makere, Kata ya Makere, inawezekana mtu huyu alikwenda kutoa taarifa za uongo za kuwa amepoteza kadi ili aweze kupata kadi nyingine,” amesema.
Jaji Mwambegele amesema mtu huyo ametenda kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, kifungu cha 114 na tayari amemwagiza Mkurugenzi wa Uchaguzi kuwasilisha taarifa hizo Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Amesema tathmini iliyofanyika kwenye maeneo ambayo wameanza kuandikisha, ni kuwa baadhi ya watu hufika vituoni na kutoa taarifa za uongo za kupoteza kadi zao ili wapate vitambulisho vipya.
Amesema wapo wananchi wenye kadi za kupigia kura zilizotolewa kwa jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao hufika vituoni kutaka kupata kadi zenye jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Amesema wenye kadi hizo na hawajahama maeneo yao ya kiuchaguzi, waendelee kuzitumia kwa kuwa kadi hizo ni halali na zitatumika kwenye chaguzi zote zinazosimamiwa na INEC.
Ameeleza kuwa katika uandikishaji, ipo mifumo miwili, ule wa kuchukua taarifa zote za wapigakura bila kutofautisha iwapo amejiandikisha mara moja au mbili au zaidi; na mfumo mwingine wa kubaini wapigakura waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwa kutumia alama za vidole, kufanana sura na kufanana kwa majina (AFIS).
Tatizo la kujiandikisha zaidi ya mara moja si geni, Jaji Mwambegele amesema kwa mwaka 2015, Tume ilibaini wapigakura 52,078 waliojiandikisha zaidi ya mara moja na mwaka 2020, watu 42,301 walijiandikisha zaidi ya mara moja na majina yao hukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo wa Tume amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Uhamiaji, kupitia maeneo ya vituo vya uandikishaji na kutoa elimu kwa mawakala wa vyama vya siasa ili kuhakikisha wananchi ambao si raia hawaandikishwi katika daftari hilo.
Wakizungumzia uandikishaji unaotarajiwa kuanza Agosti 5, 2024 mkoani Geita, wakazi wa mkoa huo wameeleza shauku yao ya kujiandikisha ili uchaguzi utakapofika, nao waweze kuchagua viongozi wao kama wananchi wengine.
Mkazi wa Geita, Ikorongo Otto, ameishauri jamii kuona jambo hilo ni la kizalendo, hivyo walione kama la kwao na linawahusu wenyewe, wasikubali kuliharibu kwa aina yoyote.
“Suala hili ni la kitaifa, linahitaji uungwana na uzalendo, Tume nayo ijipange kuhakikisha wote wanaotaka kuharibu wanachukuliwa hatua, lakini nao wajitathmini wasiache mianya itakayopelekea mtu kuandikishwa mara mbili,” amesema Otto.
Grace Mapalala, mkazi wa Mtaa wa Mission, mjini Geita, amesema yeye ni miongoni mwa watu wanaosubiri kuboresha taarifa zake kwa kuwa uchaguzi wa mwaka 2020 alijiandikisha akiwa Mwanza na kwa sasa anaishi Geita, hivyo anasubiri kufikiwa ili atimize haki yake.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.