VIKUNDI VYA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA NA WAFANYABIASHARA MTWARA WAPATIWA ELIMU YA FEDHA.

Na Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara

Vikundi vya Huduma ndogo za fedha pamoja na Wafanyabiashara mbalimbali kutoka Manispaa ya Mtwara-Mikindani, wameshiriki katika mafunzo ya utunzaji fedha yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi za Fedha pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara, na kushirikisha wafanyabiashara na wananchi zaidi ya 500 kutoka maeneo mbalimbali.

Akizungunza kwa niaba ya washiriki wenzake, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania -TWCC Mkoa wa Mtwara, Bi.Mwajuma Oankoni, alisema kuwa elimu hiyo imekuja wakati muafaka na italeta manufaa kwa wananchi.

“Mimi kama mfanyabishana na kiongozi wa wafanyabiashara wanawake katika mkoa wa Mtwara, napongeza sana juhudi hizi za serikali, elimu ya fedha inahitajika sana katika mkoa wetu kutokana na wengi wetu kufanya mambo kwa mazoea ” alisema Bi. Mwajuma

Kwa upande wake mfanyabiashara Bi. Mwajuma Issa, alisema kuwa elimu iliyotolewa itawasaidia kutunza fedha katika taasisi rasmi, ili ziweze kuwasaidia kwa matumizi ya muda mrefu.

“Sisi tumezoea mtu ukipata hela unaziingiza kwenye matumizi zote, tena matumizi yenyewe ni ya shughuli za unyago na sherehe zingine, hali ambayo imekuwa ikizidisha umasikini kwa wananchi wengi hivyo elimu hii itatusaidia kuepukana na hilo” alieleza Bi. Mwajuma

Awali akizungumzia mafunzo hayo, Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro alieleza kuwa lengo ni kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya masuala ya fedha kwa ujumla.

“Programu hii inalenga kuwafikia wananchi wengi kutoka katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara, ili pamoja na mambo mengine wafahamu maeneo rasmi ya kupata huduma za kifedha na namna ya kuzisimamia fedha zao kwa ajili ya kuwaletea maendeleo. alisema Kimaro.

Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha – Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro akitoa elimu ya fedha kwa wanavikundi na wajasiriamali katika ukumbi Shule ya Ufundi ya Sekondari Mtwara (Mtwara Technical Secondary School) Manispaa ya Mtwara.

Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonza, akitoa elimu ya fedha kwa Wanavikundi na Wajasiriamali katika Ukumbi Shule ya Ufundi ya Sekondari Mtwara (Mtwara Technical secondary school) Manispaa ya Mtwara.

Baadhi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wa Manispaa ya Mtwara wakipatiwa mafunzo ya elimu ya fedha na Wizara ya Fedha wakishirikiana na Taasisi za Fedha pamoja na OR TAMISEMI mkoani Mtwara.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha)

Related Posts