Tabora. Mianya ya upotevu wa mapato imetajwa kuwa moja ya changamoto zinazorudisha nyuma ustawi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete. Hii ni kutokana na baadhi ya wagonjwa wanaokwenda kupatiwa matibabu hospitalini hapo kutoroka bila kulipia bili baada ya kutibiwa.
Imeelezwa kuwa hospitali hiyo inapoteza zaidi ya Sh5 milioni kila mwezi kwa wagonjwa kutoroka bila kulipa bili za matibabu.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Joachim Eyembe, amesema kiasi hicho cha mapato kimekuwa kikipotea kila mwezi kwa wagonjwa zaidi ya 30 kukimbia bila kulipa bili zao.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Julai 26, 2024, Eyembe amesema changamoto hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya hospitali, jambo ambalo pia ni hatari kwa ustawi wa huduma za afya.
“Tumekuwa tukipata changamoto kwa wagonjwa kutoroka bila kulipa ankara zao wanapofika hapa na kupatiwa matibabu. Kwa muktadha huo, tumekuwa tukipoteza zaidi ya Sh5 milioni kila mwezi kwa wagonjwa kutolipa bili,” amesema.
“Mgonjwa anafikishwa hapa akiwa na hali mbaya na tunatimiza wajibu kwa kumpatia matibabu kuokoa maisha yake, lakini wanapoanza kupata nafuu na kuona hawana uwezo wa kulipa, anatokomea. Wito wetu ni kwamba wanaopewa huduma walipe ili hospitali iweze kujiendesha kwa kulipia huduma za wadau wetu wanaotupatia bidhaa kama dawa. Tunaweka mikakati kuwabaini wote na kuchukua hatua za kisheria,” ameongeza Eyembe.
Hilo pia limesisitiza na Muuguzi Mkuu katika hospitali hiyo, Mwanaid Shangi, kuwa wanatimiza wajibu wao kwa mgonjwa, lakini baadhi wamekuwa wakitoroka baada ya kupatiwa matibabu na afya yao kutengemaa.
“Mgonjwa anafikishwa hapa akiwa hajitambui na tunampa tiba inayostahiki, na anapata unafuu. Hata hivyo, wengine sio waaminifu; akipata nafuu, anatoka kama anakwenda kununua kitu nje, anatokomea moja kwa moja,” amesema Shangi.
Mkazi wa Manispaa ya Tabora, Adelah Fidelis, aliyezungumza na Mwananchi, ameeleza kuwa tabia ya wagonjwa kukimbia bila kulipa ankara hazikubaliki kwani upo utaratibu wa wasio na uwezo kupatiwa huduma za matibabu bila malipo.
“Unapotibiwa na kulipa, unarahisisha wengine kupatiwa huduma bora. Lakini, ubinafsi ukizidi, wengine hawatapewa matibabu, hivyo wagonjwa walipe bili zao,” amesema Fidelis.
Kwa upande wake, Elizayo Hubert ameomba Serikali na uongozi wa hospitali kuweka utaratibu mzuri ili kuwadhibiti wagonjwa wanaotoroka bila kulipa bili.
Hospitali ya Rufaa ya Kitete ilianzishwa mwaka 1906, wakati huo ikiwa kama kambi ya jeshi kwa ajili ya kutoa huduma za afya.
Mabadiliko hayo yaliendelea hadi baadaye ikawa Hospitali ya Jeshi na sasa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Inahudumia wagonjwa kutoka mikoa jirani ya Katavi na Kigoma na inatumia vifaa vya kisasa vya kutoa huduma za afya.