Mbeya. Wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (Must) wamepoteza maisha chini kwenye mashimo ya mgodi wa Mirerani ambako walikwenda kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi zimedai kuwa wanafunzi hao wamefariki dunia baada ya kukosa hewa ndani ya mgodi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Julai 26,2024, Ofisa Mawasiliano na Masoko wa Chuo cha Must, Dickson Msakazi amewataja wanafunzi hao kuwa ni Given Machunde ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Uhandisi Madini na Ismail Omary wa Shahada ya Uhandisi Mitambo, wote wa mwaka wa pili.
Msakazi amesema kwa taarifa za awali, chanzo cha vifo vyao ni kukosa hewa wakiwa mgodini wakiendelea na mafunzo hayo.
“Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia sana kwani bado hata mmiliki wa mgodi hawezi kusema chochote, tusubiri watu walioenda kushiriki mazishi tutakuwa na majibu lakini pia mamlaka husika baada ya kufanya uchunguzi,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi