Wananchi kaskazini waitwa kutoa maoni dira ya Taifa

Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kufungua kongamano la ukusanyaji wa maoni ya wananchi kwa ajili ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kesho Julai 27, 2024, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC).

Kongamano hilo la pili la kikanda, litakalofanyika Arusha likiwashirikisha wananchi wa kanda ya kaskazini, limeandaliwa na Tume ya Mipango kwa lengo la kukusanya maoni kwa ajili ya utengenezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo, Ijumaa Julai 26, 2024, Mjumbe wa timu kuu ya kitaalamu ya Dira ya mwaka 2050, Dk Richard Shukia amesema kongamano hilo linatarajia kuongeza uelewa wa umma juu ya dira hiyo, pia kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato huo.

“Lengo la kongamano hili kufanyika kila kanda ni ili kuwafikia wananchi wengi zaidi mubashara na kupitia vyombo vya habari, ambapo tumeshafanya Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza na sasa ni zamu ya Kanda ya Kaskazini mkoani Arusha,” amesema Shukia.

Amesema lengo la dira hiyo ni kutoa mwelekeo wa nchi hususani katika maendeleo, hivyo amewataka wananchi wa kanda ya kaskazini kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Arusha, Selemani Yusuph amesema Serikali inapaswa kujua wapi ilikwama katika dira mbili zilizopita na kutatua changamoto zilizojitokeza ili kuboresha na kufikia mafanikio iliyojiwekea katika dira mbili zilizopita.

“Katika dira za awamu mbili zilizopita ya mwaka 2005-2019 na ile ya 2020 – 2025, Serikali ilikuwa na malengo mengi ikiwemo ya kuboresha hali ya maisha ya Watanzania, lakini pia kujenga uchumi imara utakaowezesha kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine,” amesema Yusuph.

“Lakini ukiangalia hadi sasa mambo bado magumu, hali ya uchumi wa wananchi mifukoni ni mbaya, ajira bado tatizo kwa vijana ambao ni zaidi ya nusu ya Watanzania wote, hivyo nadhani Serikali ingeona wapi ilijikwaa na iboreshe kufanikisha hayo kwanza katika dira ijayo nadhani itakuwa vema sana.”

Kwa upande wake, Elizabeth John amesema Dira ya Taifa awamu ya tatu ilenge zaidi kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ili kusaidia upatikanaji wa ajira za kutosha kwa vijana, hivyo hii iboreshe mfumo wa elimu nchini.

“Tukitoa maoni kila mara bila mafanikio kuonekana itakuwa kama tunacheza, nadhani Serikali itafute ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la ajira kwa vijana kwa kufufua viwanda vingi iwezekanavyo, pia kuwaongezea vijana motisha ya uwekezaji katika nchi yao,” amesema.

Pia, ameitaka dira hiyo iboreshe mitaala ya ngazi zote za elimu itakayosaidia vijana wanaohitimu bila kujali ngazi gani, waone fursa ya kujiajiri au kushindana katika soko la ajira kimataifa.

Pia, dira imwezeshe kutumia elimu aliyonayo kufanya uwekezaji na kuajiri wengine zaidi ya kutegemea ajira za sekta ya umma ambazo haziwezi kuajiri hata asilimia 10 ya wahitimu kutoka vyuoni,” amesema Elizabeth.

Related Posts