WAZIRI MKENDA:NI MARUFUKU KUMFUKUZA MWANAFUNZI KWA KUSHINDWA KUCHANGIA MCHANGO WOWOTE

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, akizungumza katika Kongamano la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni lililofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nomboa,akizungumza katika Kongamano la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni lililofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule,akizungumza katika Kongamano la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni lililofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,(hayupo pichani)  katika Kongamano la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni lililofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, akikagua mabanda Mbalimbali wakati wa Kongamano la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni lililofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

……

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema ni marufuku Mwanafunzi yeyote kufukuzwa kwenye shule za umma, kurudishwa nyumbani kwa sababu mzazi ameshindwa kuchangia mchango wowote ikiwemo huduma za chakula.

Mkenda ametoa agizo hilo Julai 26, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza katika Kongamano la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni, akisisitiza mzazi anayekataa kuchangia mchango uliowekwa kulingana na miongozo waliyojiwekea Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaweza kuchukua hatua dhidi ya mzazi wakati Mwanafunzi akiendelea na masomo.

Akihutubia Kongamano hilo Waziri huyo amewataka Wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana kuhamasisha huduma ya chakula kwa Wanafunzi wakiwa shuleni.

“Lishe bora shuleni ni msingi muhimu katika maendeleo ya kiafya na kiakili na kwamba inachangia Mwanafunzi kujifunzaji kwa ufanisi. Mwanafunzi anapokosa chakula hukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo njaa, utoro wa rejareja na hata kukatisha masomo kwa baadhi yao” alisema Mkenda.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa kuhamasisha jamii na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na kuchangia uwepo wa huduma hii katika shule za Awali, Msingi na Sekondari.

Amesema Kongamano hilo, limewakutanisha Wataalam kutoka Wizara za kisekta Mashirika mbalimbali na Vyuo Vikuu ambao wamejadili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na Uendelezaji wa Programu ya chakula shuleni, Huduma za afya na lishe shuleni pamoja matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa na Upatikanaji wa taarifa za utoaji wa huduma ya chakula shuleni.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kusimamia na kufuatilia suala la lishe Shuleni, hali inayochochea afya na elimu bora katika mkoa huo.

Amesema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2024, Shule za Msingi za Serikali *854* zenye Wanafunzi *437,749* sawa na asilimia *70* ya Wanafunzi zimeweza kutoa huduma ya chakula na Sule za Sekondari *261* zimetoa chakula kwa Wanafunzi *143,700* sawa na asilimia *69.2*

Akitoa neno Mwakilishi wa Balozi wa Marekani Nchini Bw. Paul Alberghine ameipongeza Serikali kwa kutilia mkazo suala la chakula na lishe Shuleni, pamoja na mashirikiano mazuri kupitia Mpango wa Kimataifa wa McGovern-Dole wa Chakula kwa Elimu na Lishe ya Watoto tangu 2010.

Related Posts