Arusha. Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linamshikilia Dominick Miduriek (32) mkazi wa Oldonyokumur Kata ya Muriet jijini Arusha kwa tuhuma za kumwingilia kijana wa miaka (23) kinyume na maumbile.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema kuwa polisi bado inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
“Hilo tukio nimesikia tu juu juu tu na nadhani kuna mtu kama huyo anashikiliwa Kituo cha Muriet, ngoja Askari wangu wanafuatilia tutakachofanikiwa kupata nitakujulisha zaidi,” amesema Masejo.
Akisimulia tukio hilo, kijana huyo amesema kuwa usiku wa Jumatatu Julai 22, 2024 majira ya saa tano usiku alikuja mtuhumiwa na kumgongea mlango wake, huku akimwomba kumsaidia kusukuma pikipiki yake kuelekea nyumbani kwao.
“Huyu mtu anaishi mtaa wa pili, akaja kumuomba nikamsaidie kusukuma pikipiki yake hadi nyumbani kwao kwa madai kuwa anaogopa kuiwasha itatoa mngurumo ambao mama yake wanaoishi naye atasikia na kumgombeza kuwa anatoka wapi usiku huo” amesema kijana huyo.
Bila kujua dhamira ya mtuhumiwa, kijana anasema kuwa alitoka ili kwenda kumsaidia.
Akizungumzia tukio hilo, baba mkubwa Mathayo Mollel amesema kuwa mtuhumiwa huyo mwenye mke na watoto wawili ameidhalilisha Kabila la Kimasai ambao ni mkosi.
“Hii ni aibu na mkosi mkubwa hata kumshika tu mwenzio makalio yake licha ya kumuingilia, tunaomba serikali itusaidie kumuadhibu mtu huyu,” amesema Mollel.
Amesema kuwa katika kutaka kuficha tukio hilo, mtuhumiwa akishirikiana na mama yake wametuma wazee kuleta ng’ombe, kondoo na kreti mbili za soda kuomba msamaha kimila lakini kwa udhalilishaji huo wamegomea zaidi wanaiomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya kijana huyo.
Mjomba wa kijana aliyelawitiwa, Leaky Satiani amesema kuwa ni kweli tukio hilo limetokea na wanafanya jitihada kumhudumia.