Biteko ataka vitendo zaidi kuliko maneno Wizara ya Nishati

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka watumishi wa wizara yake na taasisi zake kuiishi kauli mbiu ya sekta ya nishati, ambayo ni maneno kidogo vitendo zaidi ili kuweza kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.

Dk Biteko ameyasema hayo leo  Julai 27, 2024, wakati wa bonanza la nishati lililowashirikisha watumishi wa Wizara ya Nishati na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Amesema sekta ya nishati ni muhimu kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi na kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anawategemea katika kutoa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.

“Nia yetu ni moja ni kuhamasishana kutoa huduma bora kwa Watanzania kwa sababu wanatutegemea. Na mheshimiwa Rais anatutegemea sisi  kutoa huduma nzuri kwa wananchi na waone uhalali wa kodi wanazolipa na wanavyohudumiwa,” amesema.

Amewataka watumishi wa wizara hiyo na taasisi hizo kupendana, kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kusukuma mbele gurudumu la nishati.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama (kushoto) akimkabidhi kombe kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko (kulia) wakati wa bonanza lilowashirikisha watumishi wa Wizara ya Nishati na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Aidha, amesema amefurahishwa na morali waliyonayo watumishi ambao walishiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali.

Ameahidi kuwa huo ndio utakuwa utaratibu wa kila mwaka mara baada ya kumalizika kwa Bunge la bajeti.

Amesema lengo ni kuhamasishana ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa Watanzania kwa sababu  wanaitegemea wizara hiyo na taasisi zake katika kupata huduma hiyo.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu , Jenista Mhagama amesema kufanikiwa kwa bonanza hilo ni mwitikio wa lengo la Rais Samia ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya njema na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema kuwa, michezo inaimarisha afya inajenga umoja, inaleta furaha na kujenga maarifa mapya ya kuwatumikia Watanzania hivyo amempongeza Dk Biteko kwa kuasisi bonanza hilo muhimu kwa watumishi.

Related Posts