Boban akimbilia Tusker Kenya | Mwanaspoti

TUSKER ya Kenya imekamilisha uhamisho wa aliyekuwa mshambuliaji wa Biashara United, Mganda Boban Zirintusa kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Msimu uliopita nyota huyo alikuwa katika kiwango bora kwenye kikosi hicho cha Mara kilichoshiriki Ligi ya Champion-ship baada ya kufunga mabao 21, ikiwa ni idadi sawa na shambuliaji nyota wa KenGold, Edgar William.

Akizungumza na Mwanaspoti, Boban alisema licha ya kupata ofa nyingi ila amevutiwa zaidi na Tusker huku akiweka wazi kujiunga kwake na timu hiyo ni jambo kubwa katika maisha yake kwa sababu ni miongoni mwa timu bora zilizopo Kenya.

“Najisikia nipo nyumbani kwetu Uganda kwa sababu mazingira hayatofautiani kwa sana. Nashukuru kwa imani kubwa niliyopata katika Ligi ya Championship msimu uliopita nikiwa na Biashara kwani ndiyo iliyonifanya kufika hapa nilipo leo,” alisema.

Boban aliongeza kuwa mojawapo wa mambo makubwa ambayo hasahau katika soka la Tanzania ni ushindani mkubwa aliokutana nao kwani mbali na Ligi Kuu Bara ambayo ameshaichezea, lakini hadi timu za madaraja ya chini  ni kivutio kikubwa.

Nyota huyo alitua Biashara United akitokea Express FC ya Uganda huku pia akichezea timu mbalimbali zikiwemo Mtib-wa Sugar ya Tanzania, Polokwane City (Afrika Kusini), Buildcon (Zambia), Ethiopian Coffee (Ethiopia) na Mohun Bagan AC ya India.

Boban ni miongoni mwa nyota wanaowania tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya mchezaji bora wa Ligi ya Championship zitakazofanyika Agosti Mosi, mwaka huu jijini Dar es Salaam akiwa sambamba na Edgar William na Casto Mhagama wote wakichezea kikosi cha KenGold.

Related Posts