CROWS imeanza visingizio baada ya kocha wa timu hiyo, Abbas Sanawe kusema kuwa, kukosa utulivu kwa wachezaji hasa katika robo ya tatu, imechangia kwa kiasi kukikubwa kufungwa na Savio kwa pointi 92-70.
Timu hiyo ilipoteza mchezo huo wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) uliopigwa kwenye Uwanja wa DonBosco Oysterbay.
Sanawe aliliambia Mwanasposti kuwa, kukosa utulivu huo ilisababisha waweze kupoteza mipira mara kwa mara katika robo hiyo.
“Kuona hivi wapinzani wetu walitumia nafasi hiyo ya uzembe tuliofanya kufunga pointi mara kwa mara na kuzidi ujanja,” alisema Sanawe.
Hadi kufikia mapumziko Savio walikuwa mbele kwa pointi 44-42.
Akizungumza mkakati waliouweka baada ya kupoteza mchezo huo, alisema kwa sasa wamejipanga kushinda michezo yote iliyokuwa mbele yao.
“Tukishinda baadhi ya michezo naamini tutashika nafasi ya nzuri itakayotufanya tucheze ligi tena mwakani,” alisema Sanawe