Dili la KibuDenis bado kidogo

MABOSI wa Simba kwa sasa wanasikilizia tu dili la nyota wa timu hiyo, Kibu Denis aliyepo Norway kwa sasa akimalizana na klabu ya Kristiansund BK kama ambavyo Mwanaspoti lilivyoripoti awali taarifa kuwa ametoroka ni zuga tu ya viongozi wa Wekundu hao kwani walikuwa wanajua kila kitu.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo ni, mabosi wa Simba wanasikilizia dili litakavyokwenda ili wapate mgao wao kutokana na ukweli walimsainisha mkataba mpya wa miaka miwili hivi karibuni, hivyo akitua KBK ni lazima wapate chao, japo inaelezwa dau la awali ni kama wamelichomolea.

Awali ilichengeshwa Kibu alitoroka kwenda Norway badala ya kutakiwa atue kambi ya Simba iliyopo Misri, lakini pekuapekua za Mwanaspoti ilinasa faili, mchezaji huyo kaondoka huku akiwa na baraka za viongozi wa juu kwani walishapokea ofa ya Wanorway mapema, ila walihofia povu la mashabiki.

Inaelezwa barua ya kuhitajiwa kwa mchezaji huyo ilitolewa mapema mwezi huu kabla ya timu kwenda Ismailia, Misri kuweka kambi ila viongozi wakaamua kukausha kwanza kupitisha kelele za mashabiki ambao bado wana hasira za nyota wawili wa zamani wa timu hiyo, Jean Baleke na Clatous Chama kutua Yanga.

Taarifa kutoka ndani ya Simba ni dau lililopendekezwa na klabu hiyo ya Norway lilionekana dogo na mabosi wa Msimbazi wamegomea mpango wa Kibu kufanyiwa majaribio kwa muda wa mwezi mmoja na kutaka anunuliwe moja kwa moja na hivyo mazungumzo nayaendelea ili kuona dili linakamilikaje.

“Kama kutapatikana muafaka ina maana Kibu atasalia huko na klabu itavuta chake, huku nafasi yake itatafutiwa mtu mwingine kabla dirisha la usajili halijafungwa,” kilisema chanzo hicho makini kutoka Simba ambayo jana kilimtangaza rasmi Ofisa Mtendaji Mpya, Uwayezu Francois Regis kutoka Rwanda anayechukua nafasi ya Imani Kajula anayemaliza muda wa kuitumikia klabu hiyo.

Kabla ya kuibuka kwa dili hili la klabu hiyo ya Norway iliyopo Ligi Daraja la Kwanza na iliyozaliwa mwaka 2004 kama Azam FC, Kibu alizua utata kwa kushindwa kutokea kambini Misri, ilipo Simba na kuonekana akila bata jijini Florida Marekani na Mwanaspoti kama kawaida lilifichua mapema kilichokuwa kinaendelea.

Ndipo zikaibuka taarifa ametoroka wakati akiandaliwa safari ya kwenda Ismailia, lakini mtu wa karibu wa mchezaji huyo alisema Kibu atarejea kuungana na timu kama dili lake litakwama.

“Niwaambie tu, kwanza Kibu hajatoroka, bali amefanya taratibu zote ndiyo maana amepata Visa na tiketi ya ndege. Mtu hatoroki hivyo na viongozi wa Simba wanajua kila kitu tangu mapema, ila hawakutaka kuweka wazi wakitaka kwanza dili likamilike, sema nyie (Mwanaspoti) mmelianika mapema,” chanzo hicho kilisema.

“Lazima atarudi nchini pia, ndipo watajua wanamalizanaje na Simba. Hawezi kuendelea kukaa Norway wakati visa yake inaisha katikati ya mwezi ujao (Agosti), atarudi na hata akipata timu huko lazima arudi kumalizana na Simba kwani sheria ziko wazi. Nasisitiza hajatoroka.”

Kibu alitua Msimbazi misimu mitatu iliyopita akitokea Mbeya City na alikuwa na msimu mzuri wa kwanza alipomaliza kama kinara wa mabao akifunga manane, kisha msimu uliofuata alimaliza na mawili na uliopita alifunga moja tu lililokuwa la kufutia machozi katika Dabi ya Kariakoo, Simba ilipolala mabao 5-1.

Related Posts