Haier yasogeza huduma Kanda ya Ziwa, yafungua duka Mwanza

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Baada ya kuingia nchini takribani mwaka mmoja uliopita, hatimaye Kampuni ya bidhaa za umeme na vifaa vya elektroniki kutoka China ya Haier, imefungua duka lake kubwa jijini Mwanza katika jengo la Rock City Mall ambalo litahudumia wateja wake wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Duka hilo limefunguliwa leo Julai 27, 2024 katika jengo la Rock City Mall, Mwanza kwa ubia na wakala wake mkuu, Kampuni ya Primina Investment, huku ikitarajia kuwafungulia fursa mbalimbali Watanzania ikiwemo ajira, biashara na kuunga mkono jitihada za serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kampuni hiyo kutoka China iliingia nchini Januari, 2023 baada ya kuidhamini klabu ya Yanga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa udhamini wa Sh bilioni 1.5 ambapo leo ikiwa ni takribani mwaka mmoja na miezi sita, imeendelea kutanua matawi yake nchini.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Meneja Mkuu wa biashara ya Haier Tanzania, Ibrahim Kiongozi, amesema lengo ni kuleta bidhaa zao karibu na wananchi na wafanyabiashara wadogo kwani wanauza bidhaa bora kwa bei nafuu.

Alisema pamoja na bidhaa za elektroniki na vifaa vya umeme wanavyouza pia wanauza majiko ya kupikia yenye ubora wa juu ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

“Kadri biashara yetu inavyokuwa tunafungua fursa kwa Watanzania, mpaka sasa tuna makawala 144 nchini na huyu (Primina Investiment) ndiye wakala wetu mkuu Kanda ya Ziwa tunafanya ubia huu kurahisisha huduma na wafanyabiashara wadogo wapate bidhaa,” amesema Kiongozi.

Meneja Mkuu wa Haier Tanzania, Liu Chi, amesema kampuni hiyo licha ya uchanga wake nchini baada ya kuingia mwaka jana lakini ni kongwe duniani kwani ina miaka 40 katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za umeme na elektroniki.

“Tunataka kutoa bidhaa bora na huduma bora kwa wateja wetu, tumeanza sasa tuna safari ndefu ya kufika maeneo mengi na tuko tayari kulikamata soko la Tanzania,” amesema Chi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Primina Investment, Priscus Kubingwa amesema baada ya kuaminiwa na Haier kuwa wakala wake mkuu Kanda ya Ziwa watakuwa wanatoa huduma zenye ueledi kwa wateja wake wote na kuwafikia kwa urahisi wafanyabiashara wadogo wanaohitaji kuuza bidhaa za kampuni hiyo ikiwemo runinga, frji, majiko ya kupikia, viyoyozi na mashine za kufulia.

Related Posts