Kikwete ataka Watanzania kukiuza Kiswahili

Dar es Salaam. Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete amewaasa wananchi kujenga tabia ya kupenda kusoma vitabu, ili kukuza uwezo wa kitaaluma na uvumbuzi wa mambo mapya na kupunguza makosa katika lugha ya Kiswahili.

Kikwete ameyasema hayo leo Julai 27, 2024 katika maadhimisho ya miaka 10 ya Watetezi wa Kiswahili Tanzania (WAKITA) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa zimepita siku 20 tangu dunia iadhimishe Siku ya Kiswahili  Julai 7.

Kikwete amesema Lugha ya Kiswahili mpaka kufikia hapo ilipo imegharamiwa, lakini Watanzania wenye lugha yao hawana tabia ya kupenda kusoma vitabu.

Hivyo amewaasa jumuiya ya WAKITA, mabaraza na wadau mbalimbali wa Kiswahili pale kuhamasisha matumizi fasaha ya Lugha ya Kiswahili.

“Kumekuwa na makosa yanayofanywa na watu katika matamshi ikiwamo kuchanganya ‘r’   na ‘l’ hii inatokana na kutokuwa na tabia ya kusoma vitabu ili kujifunza zaidi lugha,” amesema Kikwete na kusisitiza kuwa kupitia usomaji vitabu makosa hayo yatapungua.

Pia amewapongeza WAKITA katika juhudi zao za kukitetea Kiswahili kwa muongo mmoja tangu kilivyozinduliwa mwaka 2004 Zanzibar na Mama Salma Kikwete.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu “Kiswahili Sauti ya Afrika” yamehudhuriwa na waandishi wa vitabu, wadau mbalimbali wa Kiswahili nchini na nje ya nchi sambamba na uzinduzi wa vitabu mbalimbali vya Kiswahili ikiwamo ‘Hidaya ya WAKITA’ na ugawaji tuzo kwa wadau, washititi wa lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake,  Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema chuo hicho kimekuwa kikiunga mkono jitihada za kukuza na kuueneza lugha ya Kiswahili kwa kufanya utafiti, ufundishaji, ufadhili kwa wanafunzi kutoka Ghana kwa zaidi ya miaka 50 lakini pia kuandaa kongamano la Kiswahili linalotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu Cuba.

“UDSM ina mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kupitia tafiti na ufundishaji Kiswahili wageni katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) iliyo ndani ya chuo,” amesema Profesa Anangisye

Akieleza changamoto ya kubwa katika lugha ya Kiswahili mwandishi nguli na mdau wa Kiswahili, Profesa Penina Mlama amesema Serikali inafanya juhudi ya kukibidhaisha Kiswahili nchini na mataifa mengine ya nje, lakini changamoto viwango vya Kiswahili vinashushwa kwa sababu watu hawasomi vitabu.

Amesema vijana wengi wanapotumia mitandao ya kijamii huharibu lugha kurahisisha mawasiliano.

“Tujitahidi kuuza lugha ya Kiswahili kwa mataifa mengine yenye viwango na ili kupata lugha hio inabidi watu wasome ili wapate mawazo mazito,” amesema Mlama.

Aidha, ili kupiga hatua kwa wananchi kujenga mazoea ya kupenda lugha ya Kiswahili Mkurugenzi wa APE Network, Hermes Damian, ameiomba Serikali iandae bajeti ya kununua vitabu vya Kiswahili kuwawezesha wananchi kujisomea.

Related Posts