Majaliwa achangisha Sh900 milioni ujenzi wa kanisa Lindi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameendesha harambee iliyowezesha kuchangisha Sh928.67 milioni za ujenzi wa kanisa kuu tarajiwa la Mtakatifu Andrea Kagwa la Jimbo Katoliki la Lindi.

Kati ya fedha hizo Sh464.3 milioni ni fedha taslimu na nyingine kati ya hizo zimeshawekwa benki. Sh464.37 milioni zikiwa ahadi.

Awamu ya kwanza ya ujenzi huo inatarajiwa kugharimu Sh700 milioni.

Akizungumza na waumini na wadau wengine waliohudhuria harambee iliyofanyika Ruangwa mjini, leo Julai 27, 2024, Waziri Mkuu amewataka waliotoa ahadi wazikamilishe mapema ili kazi ya ujenzi isikwame.

“Ninawashukuru wote mliofika na wote waliochangia ujenzi wa kanisa tarajiwa. Ninawaomba walioahidi, wakamilishe ahadi zao mapema ili kazi ianze kwani ramani ipo, mafundi wapo tayari, wasimamizi wa ujenzi wapo,” amesisitiza.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema uamuzi wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Wolfgang Pisa kuanza ujenzi wa kanisa kuu la jimbo hilo ni utekelezaji wa maono aliyokuwa nayo tangu aliposimikwa kuongoza jimbo hilo Juni, 2022.

“Mhashamu Baba Askofu Pisa ameanza kutekeleza maono yake kupitia kaulimbiu ya ‘Ninaona kiu’ aliyoitangaza Juni 26, 2022 wakati akisimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi. Ninawaomba wana-Lindi tumpe ushirikiano kwa sababu maono yake ni endelevu. Ninawasihi tumpe ushirikiano ili aweze kutimiza hayo maono,” amesema.

Waziri mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wazazi na walezi wawe karibu na watoto na wafuatilie hatua za ukuaji wao ili baadaye wawe raia wema.

Awali, akisoma risala kuhusu mradi wa ujenzi wa kanisa tarajiwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Mhandisi Fortunatus Machibya amesema harambee  imelenga kukusanya Sh900 milioni ambazo kati ya hizo, Sh700 milioni ni za ujenzi na Sh200 milioni ni za maandalizi ya Jubilei ya miaka 25 ya upadirisho wa Askofu Pisa na miaka 50 ya Askofu mstaafu wa Jimbo la Lindi, Bruno Ngonyani.

Amesema ujenzi wa kanisa hilo unahitaji kukamilika haraka kwa sababu wakati Jimbo Katoliki la Lindi linaanzishwa mwaka 1986, kanisa lililopo lilipewa tu hadhi na hapakuwa na jipya.

“Kanisa lililopo ni dogo, ni la zamani na uwezo wake ni kuchukua watu 600 wakati matukio ya kikanisa huwa yanaleta watu zaidi ya 1,000. Tumeamua kujenga kanisa jipya lenye uwezo wa kuchukua watu 2,000 kwa wakati mmoja badala ya kufanya ukarabati na kupoteza fedha. Hili tutalijenga kwa awamu kwa miaka mitano na hadi likamilike, tunatarajia kutumia Sh6.6 bilioni,” amesema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu Titus Mdoe, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Tellack na viongozi mbalimbali wa mkoa huo.

Related Posts