Mbeya. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa ameagiza halmashauri 45 zilizopitiwa na mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (Tactic), kujiendesha kupitia masoko na vituo vya mabasi ili kuongeza mapato.
Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Julai 27, 2024 mkoani hapa wakati akishuhudia utiaji saini ujenzi wa mradi wa stendi ya mabasi eneo la Old Airport, Soko la Matola na barabara yenye urefu wa kilometa saba vyenye thamani ya Sh 30.12 bilioni.
Mradi huo umelezwa utatekelezwa kwa miezi 12 chini ya mkandarasi mshauri Consult na kusisitiza halmashauri husika kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kukamilisha kwa wakati.
“Mbeya ni moja ya miji 45 iliyonufaika na mradi ya masoko, stendi ya kisasa ya mabasi na barabara vyenye thamani ya Sh1.1 trilioni ambayo itakuwa na tija ya kuongeza mapato kwa halmashauri husika,” amesema.
“Niagize mkandarasi mshauri kutekeleza mradi huo kwa wakati na kuzingatia muda uliopangwa kwani Serikali imeleta miradi hiyo ya kimkakati kwa makusudi na sio bahati mbaya,” amesema.
Wakati huo huo ameagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kuitisha mikutano ya hadhara ya wananchi kuelekeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiwasisitiza kuwa na jukumu zito.
“Niwatake wana Mbeya mshikamane, kwani Jiji la Mbeya linakwenda kuwa la kisasa litakutanisha mataifa mbalimbali katika shughuli za kiuchumi na kusisitiza viongozi kushirikiana ili kufikia malengo ya Serikali.
“Tukio hili kwa mkoa wa Mbeya halijaja kwa bahati mbaya, bali ni msukumo wa Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson kuwasilisha maombi serikalini kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Tamisemi,” amesema.
Amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya John Nchimbi kuendelea kudhibiti mianya ya rushwa kwa kutosita kwani Serikali ya awamu ya sita imeona utendaji wake wa kazi
“Wakati umeteuliwa kuja Mbeya tuliletewa majungu, lakini tumeona utendaji wako wa kazi endelea kuchapa kazi, tumeona kazi zako,” amesema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura), Mhandisi Victor Seff amesema kuna miradi tisa inatekelezwa nchini ukiwemo huu wa Mbeya.
Amesema mbali ya ujenzi wa miundombinu ya soko na stendi ya mabasi, bado kutakuwa na marekebisho ya kilometa 60 za miundombinu ya barabara na mifereji iliyoharibiwa na mvua.
Naye Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kuwa Mkoa wa Mbeya ulikuwa hauna stendi, lakini sasa itapatikana.
Kuhusu soko la Matola, amesema kuwa lilikuwa la kizamani na kwamba marekebisho hayo yataleta tija kubwa huku akibainisha kwa mwaka huu wa fedha Mbeya wamepata zaidi ya Sh 38.7 bilioni.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema Serikali ya awamu ya sita imeleta maendeleo kwa vitendo kwani wamepokea miradi mingi kikiwamo kituo cha pamoja cha forodha kati ya Tanzania na Malawi.
Aidha, amesema mbali na mradi huo kuna barabara ya kiwango cha lami kutoka Chunya mjini mpaka Makongorosi sambamba na ufungwaji wa miundombinu ya taa katika maeneo mbalimbali.