Mkutano Mkuu Chaneta kufanyika Arusha

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Netiboli nchini (CHANETA) utakaoafanyika Jumanne ijayo jijini Arusha.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Chaneta, Shy Rose Bhanji mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe watatu kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara.

Shy Rose alisema mbali na kufungua mkutano huo, Waziri Ndumbaro pia atafungua mashindano ya Klabu Bingwa ya mchezo huo.

“Tunaishukuru sana serikali kwa kufanikisha mkutano, huu kupitia wizara ya michezo na Baraza la Michezo na wadhamini mbalimbali, mkutano huu utahudhuriwa na wajumbe watatu kutoka kila mkoa wa Bara,” alisema Shy Rose na kuongeza;

“Mkutano huu utafunguliwa na Waziri Ndumbaro ambaye kimsingi amekuwa mtu muhimu kuhakikisha Chaneta kila kitu kinakwenda sawasawa na utakuwa ni wa siku moja. Baada ya mkutano Waziri Ndumbaro atafungua pia mashindano ya klabu bingwa ya Netboli, yatakayoanza kuanzia Agosti 1-8.”

Shy Rose alizitaja timu shiriki 13 ambazo ni; Chuo Kikuu cha Kampala Tanzania, Tamisemi, Magereza, Uhamiaji, Mapinduzi, Jeshi Stars, Mbweni JKT, Bandari, Eagle Queens, Nyika, Mbeya UWASA, Katavi na Polisi Manyara.

Chaneta imepata shavu kwa kudhaminiwa na Serena Hoteli na Ofisa Mauzo na Masoko wa Tanzania, David Sem alikabidhi hundi ya Sh25 Milioni kufanikisha mkutano na mashindano hayo.

Related Posts