2010 Lamine Yamal alikuwa ana miaka mitatu, wakati Andres Iniesta alipofunga bao la ushindi la Hispania dakika ya 116 katika Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi pale Soweto, Afrika Kusini.
Lamine alikuwa na miaka 12 tu, wakati dunia ilipokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19 maarufu kama Corona. Wakati dunia ikisumbuliwa na Covid yeye alikuwa anacheza nje ya nyumba yao akiwa hana wasiwasi.
Leo anaishangaza dunia. Ni miongoni mwa watoto wa miujiza katika soka ambao tumewahi kuletewa? Ni jambo la kusubiri na kuona. Majuzi alikuwa Ujerumani akijaribu kuithibitishia dunia kwamba yeye ni mtoto wa miujiza katika soka.
Kuna wachezaji wengi ambao walikuwa katika michuano ya Euro ambao wangeweza kumzaa. Pepe ni mkubwa kuliko baba yake Lamine. Jesus Navas ni mkubwa kuliko baba yake Lamine. Kumbe hawa wote na wengineo wangeweza kumzaa Lamine. Lakini alikuwa nao katika michuano ya Euro.
Lamine ametuchanganya wengi. Sio kwa kipaji chake pekee, bali pia kwa umri wake. Kuna wachezaji wengi wamefanya makubwa, lakini wakati wakiwa walau wametimiza miaka 21. Lamine anajaribu kutuambia kwamba anaweza kuwa Pele mpya. Kwamba anaweza kuwa Lionel Messi mpya. Kwamba ndani ya umri mdogo anaweza kufanya mambo makubwa na kisha kuyafanya kwa muda mrefu.
Pele aliwachanganya Wabrazili akiwa na miaka 15 tu pale Santos. Wakati huo mpira ulikuwa dunia nzima. Santos walikuwa wakubwa kama walivyo Real Madrid. Haikujalisha kama walikuwa Amerika Kusini au Ulaya.
Miaka miwili baadaye akaichanganya dunia akiwa na umri wa miaka 17, wakati alipokwenda Stockholm, Sweden na kutwaa Kombe la Dunia huku akiwa staa wa timu ya Brazil. Ni tofauti na Ronaldo de Lima ambaye alikwenda Kombe la Dunia pale Marekani mwaka 1994 kwa ajili ya kutazama tu.
Wapo vijana ambao walimalizia safari zao na kuwa wakubwa kuwahi kutokea. Hawa kina Lionel Messi. Lakini nawafahamu wapo ambao waliishia njiani kwa sababu tofauti. Lamine yupo tayari kuendeleza shoo zake za Euro na kisha pale Barcelona? Ni swali la kujiuliza.
Kuna mtoto pale Celtic ya Scotland aliibuka na kutinga kikosi cha kwanza akiwa na miaka 13. Alikuwa anafanya mambo ya hatari. Anaitwa Karamoko Dembele. Leo anacheza katika Klabu ya Brest ya Ligi Kuu Ufaransa akiwa mchezaji wa kawaida. Ana miaka 21.
Hata hivyo, Lamine tayari ameshafanya mambo makubwa kuliko hawa kina Karamoko. Ametwaa Euro akiwa kama staa mkubwa. Miaka 17 ilimkuta akiwa katika michuano hiyo. Je atafanya mambo makubwa au anaweza kuzama taratibu.
Kuna watu wa kuwakumbuka. Mfano mkubwa ni Neymar. Aliwahi kudai kwamba Neymar ni shujaa wake katika soka. Hata hivyo, Februari mwakani Neymar anatimiza miaka 33 na hajawahi kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia.
Sawa, kuna mahala ambapo Neymar alifika na hadi leo Lamine hajafika, lakini watu tulikuwa tunamtazama Neymar mbali. Tuliamini atafika kule ambako mboni za macho yetu hazitaweza kufika. Hata hivyo, nakukumbusha tena, Neymar hajawahi kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia.
Desemba 20, Kylian Mbappe atatimiza miaka 26. Nawakumbusha kwamba Mbappe hajawahi kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Sio kwa bahati mbaya. Sawa amewahi kutwaa Kombe la Dunia, lakini hajawahi kuwa na tuzo yake binafsi kama mwanasoka bora wa dunia.
Mwisho wa siku wanasoka mahiri huwa wanahesabiwa kwa tuzo binafsi walizotwaa na mataji binafsi waliyotwaa. Tuzo inakuwa kitu binafsi zaidi, lakini mataji mnaweza kushinda watu wengi kwa pamoja. Leo tunapozungumza Vinicius Junior anaweza kuwa mwanasoka bora wa dunia kabla ya Mbappe licha ya kwamba hajawahi kushinda taji la mwanasoka bora wa dunia na Mbappe amewahi kushinda.
Mpira upo katika mahakama ya Lamine. Ni mwanzo wa shoo yake ambayo itaishia mpaka mwisho au inaweza kukatika ghafla njiani? Hadi sasa naamini shoo zake zinaweza kufika mpaka mwisho na kama akifanya hivyo, basi utakuwa mwendelezo mpya wa mambo mapya.
Kwa mfano, Hispania itakuwa haijawahi kutoa staa mpya mwenye asili ya nje kama yeye. Baba yake ametokea Morocco, mama yake ametokea Guinea. Ni kama ilivyo kwa Mbappe ambaye baba yake ametoka Cameroon wakati mama yake ametoka Algeria.
Ni mwendelezo wa watu weusi wenye vipaji kuendelea kuiteka Ulaya. Walianza kina Zinedine Zidane, lakini kila siku inaendelea kusambaa. Sikumbuki kama Hispania ilikuwa na watu wengi kutoka Afrika katika timu ya taifa. Hawa kina Lamine na rafiki yake Nico Williams ni mwendelezo wa hatari ambao umeendelea kuibuka.
Lakini hapohapo naweza kumpa Lamine changamoto nyingine. Ameikuta Barcelona yake ikiwa chini. Haina pesa. Hapa miaka ya karibuni imechukua wachezaji wengi kwa mkopo. Anaweza kuibeba mgongoni peke yake? Waingereza wanaita ‘singlehandedly’. Akifanya hivyo atakuwa shujaa.
Atawakumbusha wengi namna ambavyo Diego Maradona aliibeba Argentina peke yake katika Kombe la Dunia 1986 pale Mexico. Lakini pia atatukumbusha namna ambavyo Maradona aliibeba Napoli mgongoni mwake miaka ya 1990 wakati ikiwa chini. Singlehandedly.
Lakini bila ya kusahau ni kwamba hawa rafiki zetu wanaoishia Lionel Messi na Cristiano Ronaldo walikuwa wametwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia wakiwa vijana zaidi. Mbappe anafikisha miaka 26 akiwa hajatwaa. Vipi kwa Lamine? Atatwaa mapema zaidi kama ilivyo kwa kina Ronaldo na Messi. Tusubiri.