UONGOZI wa Coastal Union uko katika hatua za awali za kuachana na kocha mkuu wa timu hiyo, Mkenya David Ouma, huku Abdihamid Moallin wa KMC akitajwa kwenda kuchukua mikoba kwa ajili ya msimu ujao.
Mbali na mchakato huo wa kusaka kocha mkuu, tayari kikosi hicho kimemuongeza aliyekuwa kocha wa Fountain Gate, Ngawina Ngawina ili awe msaidizi.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal, kimeliambia Mwanaspoti kwamba mabosi wa timu hiyo wana mpango wa kuachana na Ouma aliyeibeba msimu uliopita hadi kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara na kukata tiketi ya michuano ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikifika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
“Ni kweli kuna mchakato wa kuachana na Ouma kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu. Sitaweza kuweka wazi, lakini mpango ndio huo na tayari tumeanza mazungumzo na makocha mbalimbali kwa ajili ya kuziba pengo lake,” kilisema chanzo cha taarifa hizo na kuongeza:
“Hadi sasa ni makocha zaidi ya watano tupo nao kwenye mazungumzo miongoni mwao ni Moalin, Denis Kitambi na Melis Medo, raia wa Marekani na muda ukifika jina la kocha litafahamika. Mchakato bado unaendelea ikiwa ni pamoja na mazungumzo.”
Chanzo hicho kililithibitishia Mwanaspoti kuwa mabadiliko yatafanyika na wanatambua umuhimu wa kutafuta kocha mwenye vigezo kutokana na kwamba wanatarajiwa kushiriki michuano ya kimataifa hivyo hawatafanya makosa kwenye hilo.
Hata hivyo, Mwanaspoti lilimtafuta Katibu Mkuu wa Coastal, Omar Ayoub kuthibitisha taarifa hizo aliyesema dunia itawashangaa endapo wataachana na Ouma aliyeipa mafanikio timu hiyo kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
“Hizo taarifa hazina ukweli wowote labda mwakani kwa sasa kocha yupo Pemba anaendelea kukinoa kikosi chetu ambacho kinaendelea na maandalizi ya msimu mpya na michuano ya kimataifa,” alisema Ayoub.
Wakati huohuo, Ngawina ambaye tayari amemalizana na Coastal Union akiwa kocha msaidizi alisema ni furaha kubwa kwake kupata nafasi ya kufundisha kikosi hicho huku akivutiwa na mradi wa vijana uliopo.
“Mimi ni muumini sana wa soka la vijana na hata ukiangalia timu ambazo nimefundisha nimekuwa nikitoa sana nafasi kwao, kwa sababu ndio kizazi kijacho. Ukiangalia project (mradi) huu upo hapa Coastal, hivyo najivunia kuwa sehemu hiyo,” alisema.
Coastal imejichimbia Pemba ikiwa ni maandalizi ya mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam itakayopigwa Agosti 8 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.