Rais Samia ataka utafiti kutatua changamoto za usalama

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kukiwezesha Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kuhakikisha kinakuwa kituo bora cha tafiti zitakazotatua changamoto za kiusalama duniani.

Ametoa ahadi hiyo akieleza Afrika na dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama na tafiti ndizo zitakazokuwa jawabu.

Kauli ya Rais Samia imetolewa katika kipindi ambacho chuo hicho kimetambuliwa kuwa kituo cha utafiti wa masuala ya ulinzi wa kimkakati Afrika.

Rais Samia amesema hayo jijini Dar es Salaam leo, Jumamosi Julai 27, 2024 alipohutubia kwenye mahafali ya 12 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).

Amesema kuna umuhimu wa kufanyika utafiti mwingi ili kupatikana jawabu la changamoto za kiusalama kwa mataifa mbalimbali duniani.

“Serikali itakiwezesha chuo kiwe kituo mahiri cha utafiti wa masuala ya ulinzi wa kimkakati ili kutatua changamoto zilizopo,” amesema.

“Ni muhimu kuwekeza kwenye utafiti na kushirikiana na washirika ili kupata matokeo tarajiwa,” ameongeza Rais Samia.

Tafiti hizo kwa mujibu wa Rais zinapaswa kuja na mbinu rahisi za kutatua changamoto badala ya kutumia mabavu.

Amesema baada ya mafunzo hayo ni muhimu kuendeleza ushirikiano wa Afrika hasa katika sekta mbalimbali, ikiwemo masuala ya usalama.

“Baada ya mahafali tafadhali badilishaneni namba, badilishaneni uzoefu na uwezo ili kurahisisha kutatua changamoto zetu,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akishiriki mahafali ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kozi ya 12 kwa mwaka 2023/2024, Kunduchi Jijini Dar es Salaam, leo Julai 27,2024.

Pia amesisitiza uongozi wa chuo hicho kuhakikisha idadi ya wanawake wanaodahiliwa kusoma chuoni hapo inaongezeka.

Agizo hilo linatokana na alichoeleza idadi ya wanawake waliohitimu katika muhula wa 12 ni saba kati ya wahitimu 57.

Hata hivyo, idadi hiyo imeongezeka kutoka wawili waliokuwapo muhula wa 10 mwaka 2022.

“Hii nawapa changamoto mhakikishe katika nyakati zijazo, kati ya wanaodahiliwa kusoma kozi ndefu, wanawake waongezeke,” amesema.

Amewataka wahitimu kuhakikisha wanatumia taaluma walizopata chuoni hapo katika mataifa na maeneo yao ya kazi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo, Meja Jenerali Wilbert Ibuge amesema mahafali hayo yamehusisha wahitimu 57.

Kati yao, amesema 10 walikuwa wanasoma Stashahada ya Mafunzo ya Usalama na Stratejia, wengine wakiwa wa Shahada ya Uzamili.

“Wahitimu hawa walianza masomo Septemba mwaka jana na wanatarajia kumalizia Septemba mwaka huu. Hizi ni kozi za miezi 10,” amesema.

Related Posts