Dar es Salaam. Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam, Faraji Ngukah ameieleza Mahakama, jinsi mshtakiwa Baraka Mukama alivyomuita na kumwambia kuwa amsaidie ili askari wasimpeleke Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwani itakuwa shida kubwa kwake kwa sababu yeye sio wakili bali ni kishoka.
Ngukah amedai kuwa Mukama alimwambia kuwa yeye ni kishoka na anatumia jina la Baraka Mukami ambaye ni daktari na mhadhiri wa chuo cha Dodoma, hivyo aliomba asipelekwe Polisi.
Mukama, anakabiliwa na mashitaka mawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambayo ni kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa na kuzuia watumishi wa umma kufanya kazi yao.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kujitambulisha mahakamani hapo kuwa yeye ni wakili wa utetezi na kisha kuwatetea washtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi namba 99 ya mwaka 2019 wakati akijua kuwa hana sifa hizo.
Ngukah, ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo ya jinai namba 177/2023, ametoa maelezo hayo jana, Julai 26, 2024 , wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Asiat Muzamiru, Ngukah alidai Mei 23, 2023 asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akiendesha kesi ya jinai namba 99/2019 inayomkabili mshtakiwa Khalid Somole na wenzake watatu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya, mshtakiwa alijitambulisha kuwa anawawakilisha mshtakiwa wa pili na watatu katika kesi hiyo.
Ngukah amedai katika kesi hiyo, washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 16 yakiwamo ya kughushi stika za dawa zilizoisha muda wake na shtaka moja la kula njama ya kutenda makosa ya kughushi.
“Washtakiwa hao wanne walikuwa na uwakilishi ambapo mshtakiwa wa kwanza na wanne walikuwa wanatetewa na wakili Agatha Fabian, wakati mshtakiwa wa pili na wa tatu wao walikuwa wanatetewa na mshtakiwa ambaye alijitambulisha kuwa ni wakili Baraka Mukami” amedai Ngukah.
Ameendelea kudai kuwa siku hiyo, kesi iliitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini aligundua mshtakiwa wa tatu hakuwepo mahakamani na wala hakuwa ametoa taarifa ya kutokuwepo kwake mahakamani hapo kwa upande wa mashtaka.
“Katika kesi hiyo, nilikuwa mimi na mwenzangu Agness Mahinga na upande wa mashtaka siku hiyo hatukuwa na shahidi, hivyo tuliomba kuahirisha kesi hiyo na kuiomba mahakama itoe hati ya kumwita mshtakiwa wa tatu ili aje ajieleze sababu za kushindwa kufika mahakamani kusikiliza shauri lake” amedai Ngukah.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo kwa hakimu, Mukami alipinga maombi hayo na badala yake aliomba mahakama ifute kesi hiyo kwa kuwa upande wa mashtaka wameshindwa kuleta shahidi.
Mukami aliomba Mahakama iwafutie wateja wake kesi hiyo chini ya kifungu 225(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai (CPA).
“Upande wa mashtaka tulipinga maombi ya Mukami ya kufutiwa kesi washtakiwa na baadala yake, tuliomba mahakama itupe muda ili tuweze kufanya uamuzi” amedai wakili Ngukah.
Hata hivyo, amedai wakati wakiendelea na shauri hilo, mshtakiwa huyo alikuwa anajitambulisha kama wakili Baraka Mukami.
Aliendelea kudai kuwa baada ya muda, hakimu Mbuya alitoa uamuzi na kueleza kuwa anakubaliana na maombi ya Mukama na kuifuta kesi hiyo kupitia kifungu hicho.
Amedai baada ya washtakiwa hao kufutiwa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulielekeza askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo kuwashikilia washtakiwa hao ili waweze kukata rufaa ya kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo.
Aliendelea kudai kuwa baada ya upande wa mashtaka kutoa maelekezo hayo, PC Mubaraka alitoka chumba cha mahakama na kwenda kuwaita wenzake ili kuongeza nguvu.
“Wakiwa katika zoezi la ukamataji washtakiwa, Mukami aliwafuata askari hao ambao ukamataji huo ulikuwa unafanyika katika lango (geti) la kuingia mahakamani na kisha kumkaba mmoja wao” amedai.
Mshtakiwa alifika getini hapo na kuanza kuwasukuma askari huku akiwaambia wawaachie wateja wake na kumjeruhi askari Pc Mubaraka upande wa kiwiko cha mkono wa kushoto na upande wa kulia kupata michubuko.
Wakati Mukami anamkaba askari, wakili Agatha yeye hakuwepo eneo hilo.
Amedai baada ya kupata taarifa kuwa kuna wakili anapimana ubavu na askari, alitoka mahakamani na kwenda kuangalia nini kinaendelea katika geti la kuingia mahakamani hapo.
Pia amedai kuwa kutokana na vurugu aliyofanya mshtakiwa huyo, ilisababisha mshtakiwa mmoja kukimbia, huku wengine wakikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi.
“Baada ya kupata taarifa ya mshtakiwa mmoja kukimbia, niliagiza Mukama akamatwe na awekwe mahabusu wakati hatua nyingine zikifanyika” amedai.
Amesema kuwa akiwa bado mahakamani, Pc Mubaraka alimfuata na kumwambia kuwa yule waliyemkamata anaomba aonane na wakili aliyekuwa anaendesha kesi iliyofutwa.
“Nilienda na kumkuta Mukami amewekwa chini ya ulinzi wa polisi , na aliniambia kuwa anaomba nimsaidie askari polisi wasimpeleke kituo cha Polisi kwani itakuwa shida kubwa maana yeye sio wakili bali ni kishoka.
“Mshtakiwa alinieleza jina lake halisi ni Baraka Mukama na sio Mukami, hivyo mimi nilimueleza kuwa nimemsikia na nitawaeleza mabosi wangu kwa sababu alikuwa chini ya ulinzi, hivyo niliamini taratibu zingine zingefuata” amedai Ngukah.
Amedai Mei 30, 2023, akiwa mahakamani anaendesha kesi, alifuatwa na askari aitwaye Stephano na kuelezwa kuwa anatakiwa kuchukuliwa maelezo.
Hata hivyo, shahidi huyo alimtambua mshtakiwa na kuomba maelezo yake yatumike kama kielelezo katika kesi hiyo.
Hakimu Swallo baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15, 2024 itakapoendelea na ushahidi.Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.