WAKATI Simba ikijiandaa kurejea nchini mapema wiki ijayo ikitokea kambi ya jijini Ismailia, Misri taarifa kutoka kambi ya timu hiyo ni, mabosi wa klabu hiyo wamerejea tena kuzungumza na winga Ellie Mpanzu aliyepo AS Vita ili kuziba pengo la Kibu Denis aliyepo kwenye dili la kuuzwa Norway.
Awali ilielezwa Simba iliamua kuachana na Mkongomani huyo na kumresha Willy Onana anayetajwa kuwa mbioni kutua Qatar alipopata timu ya kuichezea, ili kukidhi idadi ya nyota wa kigeni inayotaka timu moja kuwa na wasiozidi 12.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka kwa klabu hiyo, endapo Simba itakamilisha dili la Mpanzu, basi Onana anaweza kumpisha kama itashindikana kwa Mcameroon huyo kwenda Qatar, atakayeliwa kichwa ni Freddy Michael.
“Tumerejea tena kwa Mpanzu, ambaye tunaamini ni winga mwenye kasi na mwepesi kama alivyokuwa Kibu, ingawa ishu ya Kibu bado haijaisha, kwani timu anayotaka kujiunga nayo, imnunue na sio kwenda kucheza kwa mkopo au kumfanyia majaribio ya mwezi mmoja,” chanzo hicho makini kiliiambia Mwanaspoti na kuongeza;
“Ni kweli dau la Mpanzu ni kubwa na ndilo lililoturudisha nyuma, lakini tunapambana, ili kukamailisha usajili huo, kwa vile tunaweza tusiwe na Kibu kikosini na tunaamini anaweza akaisaidia timu kwa ukubwa.”
Chanzo hicho kilisisitiza, chochote cha usajili wanachokifanya, kocha mkuu Fadlu Davis anakitambua na anafuatilia, kuhusu Mpanzu anamuona ni mchezaji mzuri.
“Kocha anajua kinachoendelea na amemuona ni mchezaji mzuri, ndio maana tumeongeza nguvu ya kuhakikisha tunampata anakuwa sehemu ya kikosi chake,” kilisema chanzo hicho.