Ujenzi wa mji wa Kitalii Serengeti Smart City kuanza hivi karibuni

Na Malima Lubasha, Serengeti
Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, ipo mbioni kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Mji wa Kitalii maarufu kama Serengeti Smart City. Mradi huu utakuwa na miundombinu mbalimbali ya kisasa itakayokidhi hadhi ya utalii wa kimataifa, ili kuvutia wageni kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Dk. Vicent Mashinji, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti ambaye amehamishiwa Wilaya ya Manyoni, amesema hayo wakati akifunga tamasha la utalii wa kitamaduni lililofanyika katika viwanja vya Right to Play mjini Mugumu. Katika tamasha hilo, aliweza kujionea vivutio mbalimbali vya kitamaduni kutoka kwa wajasiriamali na vikundi vya ngoma za asili.

Dkt. Mashinji amesema kuwa ujenzi wa mji huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, unalenga kuhamasisha utalii ambao utaingiza fedha nyingi za kigeni kutoka kwa watalii wa mataifa mbalimbali wanaotembelea Hifadhi ya Serengeti. “Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inachangia asilimia 47 ya pato la Taifa na kusaidia kuinua uchumi wa wananchi wa Tanzania. Hivyo, nawaomba wananchi tuilinde hifadhi hiyo kwa faida ya vizazi vijavyo,” alisema Dk. Mashinji.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya aliwaonya wananchi kuacha vitendo vya ujangili kwani vitendo hivyo vinaweza kusababisha watalii wasifike katika wilaya yao kuja kuona vivutio mbalimbali vilivyomo hifadhini na mji wa Mugumu. Amesema kipindi hiki wilaya inapokea watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja kutembelea Hifadhi ya Serengeti kuona wanyama, hususan nyumbu wanaohama kwenda nchi jirani ya Kenya kisha kurudi Tanzania.

Dk. Mashinji alibainisha kuwa upo utalii wa aina mbalimbali kama vile utalii wa picha, kutembea, uvuvi, mikutano, na utalii wa kitamaduni, huku akiwahimiza wananchi kutembelea hifadhi yao ya Serengeti na kuona vivutio vilivyomo na kuilinda.

“Naomba wananchi wote muwe walinzi wa Hifadhi ya Serengeti, mpige vita vitendo vya ujangili na kuua wanyama kwani hali hiyo itarudisha nyuma jitihada za kuhifadhi rasilimali zilizomo. Tuilinde na kuitunza hifadhi yetu kwa hali na mali ili watalii zaidi waje kuona vilivyomo,” alisisitiza Dk. Mashinji.

Mkuu huyo wa Wilaya aliendelea kusisitiza kuwa mji huo wa Serengeti Smart City utakuwa na miundombinu ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa inayovutia watalii. Kampeni iliyopo sasa ni kuhakikisha mazingira ya usafi katika mji wa Mugumu yanakuwa safi ili kuvutia watalii zaidi.

Related Posts