Wakili mwingine aiburuta TLS kortini

Mwanza. Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetoa siku tano kwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Baraza la Uongozi la TLS, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuwasilisha kiapo kinzani na majibu ya hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na wakili Steven Kitale.

Shauri hilo namba 17558/2024, limeitwa jana Julai 26, 2024, mbele ya Jaji Wilbert Chuma, huku mleta maombi (Kitale) ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Uongozi la TLS akiwakilishwa na mawakili zaidi ya 20 wakiongozwa na Steven Makwega, Erick Mutta na Godfrey Basasingohe.

Wajibu maombi wa kwanza hadi wa tatu wanawakilishwa na wakili, Leonard Magwayega (aliyekuwepo mahakamani), Hekima Mwasiku na David Shiratu (hakuwepo). Mjibu maombi wa nne (AG) amewakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Lameck Merumba.

Katika shauri hilo, Kitale anahoji uamuzi wa chama hicho kupandisha ada za wanachama wake kuhudhuria mkutano mkuu wa mwaka  kutoka Sh118,000 hadi Sh200,000, akidai anapoomba mihtasari ya vikao vilivyopitisha ongezeko hilo, amekuwa akipigwa danadana jambo lililomkwamisha asitekeleze wajibu wake kwa wanachama.

Pia anaiomba mahakama kutoa amri kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TLS na Baraza la Uongozi la chama hicho kutoa nyaraka za mihtasari ya vikao vilivyopitisha gharama hiyo, kikao kilichoipitisha Kamati ya Uchaguzi ya TLS na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, jambo analodai kuna ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi huo.

Wakili wa wajibu maombi, Leonard Magwahega ameiomba mahakama kuahirisha usikilizwaji wa maombi hayo, akidai wajibu maombi wote hawajawasilisha kiapo kinzani na majibu ya hoja zilizoibuliwa na mleta maombi, akitaja sababu kuwa ni ufinyu wa muda tangu wapatiwe wito wa mahakama.

“Tunaiomba mahakama kuridhia ombi letu la kutuongezea muda wa kuwasilisha viapo kinzani na majibu ya hoja za mleta maombi kwa sababu tulipokea wito wa mahakama Julai 23, mwaka huu. Bado tuko ndani ya muda wa siku 14 za kisheria za kufanya hivyo,” amedai.

“Lengo ni haki ipatikane kwa pande zote na tunaona endapo tusipopewa muda wa kufanya, hivyo huenda upande wa wajibu maombi usitendewe haki. Hivyo tunaiomba mahakama kuzingatia ombi letu,” ameomba Magwayega.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa mleta maombi, Makwega amedai wajibu maombi wameshindwa kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwasilisha viapo kinzani na majibu hayo kutokana na uzembe, hivyo ameomba usikilizwaji wa shauri hilo uendelee kwa upande mmoja.

Amedai endapo usikilizwaji wa shauri hilo hautafanyika ndani ya muda huenda haki isitendeke kwani shauri linalenga kuhoji gharama za mkutano mkuu unaotarajiwa kuanza Agosti Mosi mwaka huu, hivyo kuliahirisha huenda kukaondoa mantiki ya ufunguaji wake.

“Tuliwafikishia samansi ndani ya muda, tulitarajia kwamba kwa sababu wana mawakili wengi basi wangewasilisha viapo na majibu kwa wakati lakini hadi tunaingia mahakamani hakuna aliyefanya hivyo,” amedai.

Ameiomba mahakama shauri hilo liendelee na usikilizwaji wa upande mmoja.

Baada ya pande hizo mbili kuvutana kwa hoja kwa takribani saa 2.30, Jaji Chuma aliahirisha shauri hilo hadi saa 10.30 jioni aliporejea mahakamani na kusoma uamuzi.

Jaji Chuma amesema baada ya mawasilisho ya pande zote hakuna ubishi kwamba wajibu maombi walipokea samansi na bado shauri hilo liko ndani ya muda kwa mujibu wa sheria, hivyo akaamuru wajibu maombi kuwasilisha viapo kinzani na majibu ya hoja za mleta maombi mahakamani hapo kabla ya Julai 30, 2024 saa 2.30 asubuhi.

“Lengo ni kutenda haki kwa kila upande na mahakama inaamuru wajibu maombi wafanye hivyo, baada ya kutekeleza maelekezo hayo, tutaendelea na usikilizwaji wa shauri saa 7.00 mchana siku hiyohiyo,” amesema Jaji Chuma.

Related Posts