WANANCHI TANDAHIMBA WAFIKIWA NA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha – Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa elimu ya fedha kwa wanavikundi na wajasiriamali Mkoani Mtwara.

Na Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara

 

Wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Halamshauri ya Wilaya ya Mtwara, wameendelea kupata elimu ya matumizi sahihi ya fedha ambayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha, yakihusisha Wilaya zote za mkoa wa Mtwara

 

Katika mafunzo yaliyofanyika katika Kijiji Cha nanhyanga, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, wajasiriamali na wafanyabishara  walijitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo huku wengi wao wakikiri kuwa wamejifunza mambo mengi ambayo walikuwa hawayajui kabla.

 

Akizungumzia programu hiyo, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha – Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, ameeleza kuwa Wizara ya Fedha inafanya jambo ambalo lilihitajika kwa wananchi kwa muda mrefu akisisitiza kuwa sasa kutakuwa na mwamko mpya.

 

“Wananchi hususan wa maeneo ya vijijini wanatakiwa kuwa na uelewa wa masula muhimu ya fedha, ndio maana unaweza kukuta wana fedha nyingi kwa wakati mmoja na baada ya muda hamjui hata zilienda wapi, kupitia elimu hii itawakomboa” alisema Bi. Mnzava.

 

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha – Wizara ya Fedha, Bw. Kelvin Kalengela, amesema Mkoa wa Mtwara unakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa matumizi ya fedha kwa wananchi wake, na ndio maana wengi wao wamekuwa wakienda kukopa mikopo inayowaumiza.

 

“Kuna mikopo ya aina mbalimbali inatolewa kienyeji, mingi haina sifa wala vigezo lakini wananchi hawajui ndio maana tunawapa elimu ili pia wasitumie fedha zao vibaya” alieleza Bw. Kalengela.

 

Kwa upande wake Bi Habiba Shube Mwananchi wa Kijiji cha Tandahimba ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Taasisi zingine zinazoshiriki katika kutoa elimu hiyo akieleza kuwa itawasaidia wananchi hususan akina mama kuepuka mikopo umiza.

 

“Hii sisi akina mama naweza kusema inatuhusu kuliko hata wanaume, sisi ndio wahanga wakubwa maana tuna shughuli nyingi ambazo zinatumia pesa hivyo tunajikuta tunaingia kwenye mikopo isiyo na sifa tunalipa madeni, kila siku tunalipa madeni tu” Alisema mwananchi huyo.

 

Mafunzo haya yaliyoanza mapema wiki hii, yanaendelea katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mtwara, lengo lake likiwa  ni kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya masuala ya fedha kwa ujumla.

 

 

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha – Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa elimu ya fedha kwa wanavikundi na wajasiriamali Mkoani Mtwara.

 

 

Afisa Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji na Dhamana – Wizara ya Fedha, Bw. Godfrey Makiyo, akitoa elimu ya fedha kwa wanavikundi na wajasiriamali Mkoani Mtwara.

 

 

Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Bi. Aveline Kapologwe, akitoa elimu ya fedha kwa wanavikundi na wajasiriamali Mkoani Mtwara.

 

 

Baadhi ya wajasiriamali wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba wakipatiwa mafunzo ya elimu ya fedha na Wizara ya Fedha wakishirikiana na Taasisi za Fedha pamoja na OR TAMISEMI mkoani Mtwara.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha-Mtwara.

Related Posts