Dar es Salaam. Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Stergomena Tax amesema ushirikiano wa kijeshi kati ya China na Tanzania una nafasi kubwa katika kuhakikisha dunia inakuwa salama.
Tax ameeleza hayo wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 97 ya Jeshi la Ukombozi la China (PLA) yaliyofanyika katika ubalozi wa China Jijini Dar es Salaam.
Tax amesema wakati Tanzania ikisherekea miaka 60 ya kuanzishwa kwa Jeshi lake la Wananchi (JWTZ) na China ikisherehekea miaka 97 ya PLA ni muhimu kujenga msingi muhimu kujenga uhusiano imara kwa ajili ya nchi hizo na Dunia kwa ujumla.
“Kwa pamoja tunaweza kufanya kazi ya pamoja ya kuhakikisha usalama na uthabiti wa dunia kwa kupambana na matishio tofauti ya usalama na kufanikisha malengo yetu ya maendeleo,” amesema Tax
Amesema hilo linaweza kufanikiwa kwa kuendelea ushirikiano baina ya majeshi ya nchi mbili kwa maslahi ya usalama wa dunia na kizazi kijacho.
Tax amesema uhusiano wa kimkakati kati ya China na Tanzania uliidhinishwa na wakuu wa nchi hizo mbili (Rais Xi Jinping na Rais Samia Suluhu Hassan) Janauri mwaka huu.
“Uhusiano kati ya JWTZ na PLA mpaka sasa ni mzuri kwa kiwango cha juu na utaendelea kuimarishwa siku zote,” alisema Tax huku akieleza namna ambavyo ushirikiano huo umenufaisha pande zote mbili.
Amesema mazoezi ya pamoja baina ya JWTZ na PLA pamoja na kuboresha uthabiti wa jeshi la Tanzania lakini yanatoa fursa kwa maofisa na askari wa pande zote kubadilisha uzoefu katika maeneo mbalimbali.
“Meli vita ya matibabu iliyotumwa na Jamhuri ya watu wa China si tu inaashiria mshikamano na urafiki tulionao bali uhusiano wa kweli na si ishara tu ya kitendo cha utu bali ilitoa msaada mkubwa wa matibabu yaliyohitajika kwa wananchi,” amesema.
Aidha hafla hiyo ilihudhuriwa na makumi ya maofisi na maaskari wa JWTZ na PLA watumishi na wastaafu, watumishi wa Serikali za nchi hizi mbili, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi, wanadiplomasia na waambatana wa mejeshi ya nchi tofauti hapa nchini.
Katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na Mkuu wa majeshi nchini Jenerali Jacob Mkunda, Balozi wa China nchini Mingjian Chen ameeleza namna PLA ambavyo limekuwa likihusika na kuhakikisha usalama wa dunia lakini pia ushirikiano kati ya Taifa lake na Tanzania.
“Jeshi la ukombozi wa la watu wa China liliasisiwa na chama cha kikomunisti cha China (CPC) Miaka 97 iliyopita. Limechangia katika usalama wa dunia kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na ulinzi wa amani, usindikizaji wa meli na huduma za kibinadamu ikiwemo uokozi,” amesema Chen.
Ameongeza kuwa China itaendelea kuwa sehemu ya usalama wa dunia na kuchangia maendeleo huku akielezea uhusiano wake na Tanzania kama wa kuigwa.