Chomoko amng’oa Lukwele unaibu meya Manispaa ya Morogoro, asubiri kuthibitishwa

Morogoro. Diwani wa Mkundi, Seif Chomoka ameibuka na ushindi wa kura 23 dhidi ya 15 za mpinzani wake, Mohamed Lukwele katika kinyang’anyiro cha kusaka kiti cha Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, uchaguzi uliofanyika kwa ngazi ya chama.

Lukwele kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), alikuwa akitetea kiti hicho.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Julai 28, 2024, mjini hapa, Chomoka amewashukuru  madiwani wenzake kwa kuonyesha imani yao kwake, huku akisema endapo atathibitishwa na Baraza la Madiwani kuwa Naibu Meya, atajitahidi kufanya kazi kwa bidii akilenga masilahi mapana ya wananchi wa manispaa hiyo.

“Leo hii ninyi (madiwani) mmenichagua kugombea nafasi ya Naibu Meya wa Manispaa yetu ndani ya chama chetu na ikitokea nimethibitishwa kuwa Naibu Meya, nitajituma kuchapa kazi kwa kumshauri vizuri meya na kushirikiana na wataalamu wetu kusukuma gurudumu la maendeleo ili manispaa isonge mbele zaidi,” amesema Chomoka.

Diwani wa Sultani, Samuel Msuya amesema nafasi ya Naibu Meya huchaguliwa katika uchaguzi unaofanyika kila mwaka kulingana na sheria zilizopo.

“Nafasi ya Naibu Meya hugombewa kila mwaka na vyama vyote vya siasa katika halmashauri husika, lakini kabla ya kuchaguliwa, vyama vya siasa vina uchaguzi wao wa kumpata mgombea mmoja atakayeshinda dhidi ya wagombea wengine wa chama husika katika uchaguzi unaofanyika kwenye  vikao vya baraza la madiwani,” amesema Msuya.

Msimamizi wa uchaguzi huo, ambaye ni Katibu wa UWT Wilaya ya Morogoro, Judith Usaki amesema Lukwele alipata kura 15 kutoka kwa wajumbe 38.

“Kwa sababu Manispaa ya Morogoro hatuna madiwani kutoka vyama vingine vya siasa, jina la Seif Chomoka litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ili kuthibitishwa kuwa Naibu Meya baada ya wajumbe wa CCM kulipitisha katika kura za maoni,” amesema Usaki.

Related Posts