Dabi ya Kariakoo kuitesti VAR

SIKU hazigandi. Bado siku 11 tu kabla ya Simba na Yanga kuvaana katika pambano la Dabi ya Kariakoo ya Ngao ya Jamii.

Timu hizo zitakutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kukata utepe wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2024-2025, zote zikiwa zimetoka kufanya matamasha yao, Simba Day na Wiki ya Mwananchi kwenye uwanja huo huo.

Simba na Yanga zinakutana kwa mara ya nne mfululizo katika michuano hiyo tangu 2021, huku Yanga ikishinda mara mbili, 2021-2022 kwa ushindi wa bao 1-0 kisha kutakata tena 2022-2023 kabla ya msimu uliopita, Simba kujibu mapigo kwa ushindi wa penalti 3-1 baada ya dakika za kawaida kumalizika kwa suluhu.

Kwa misimu saba mfululizo tangu 2017, Simba imecheza fainali za mechi hizo na kubeba matano, huku kwa Yanga ndani ya muda huo imecheza fainali nne na kushinda mbili na nyingine kama hizo ikipoteza zote kwa Simba 2017-2018 na msimu uliopita, hivyo mechi ya Agosti 8 ambayo ni nusu fainali itakuwa ya kisasi.

Yanga kwa sasa ipo Afrika Kusini ikijiandaa na msimu mpya na leo jioni itashuka uwanjani kuvaana na Kaizer Chiefs katika mechi ya kuwania Kombe la Toyota, wakati Simba ikiwa kambini Ismailia, Misri.

Hata hivyo, taarifa mpya kwa sasa ni kwamba huenda mechi hiyo au ile ya fainali ya Ngao ya Jamii ikatumika kwa ajili ya majaribio ya Teknolojia ya Usaidizi kwa Waamuzi kwa njia ya Video (V.A.R).

Hivi karibuni, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliweka bayana kwamba TFF ilikuwa inasubiri vibali kutoka idara ya VAR ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ili ianze kutumika rasmi ndani ya Ligi Kuu Bara inayoanza Agosti 16.

Karia alikaririwa katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia hiyo iliyofanyika Kwa Mkapa, alisema tayari kuna ‘VAR kits’ mbili hadi sasa moja kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) itakayofungwa kwenye uwanja huo na nyingine kutoa Azam Media ambayo ni ‘mobile’ inayohamishika.

Sasa, taarifa kutoka ndani ya shirikisho hilo ni kwamba huenda majaribio ya teknolojia hiyo ya VAR ikaanza katika pambano la Dabi ya Kariakoo ya Ngao ya Jamii au mechi ya fainali ya michuano hiyo inayoshirikisha timu nne zikiwamo Azam na Coastal Union zitakazovaana kwanza huko New Amaan Complex, mjini Unguja Zanzibar, siku ya Agosti 8 ambapo jioni yake Kwa Mkapa ndipo Yanga na Simba zitapepetana.

Teknolojia hiyo ya VAR ilianza rasmi kutumika mwaka 2016 na Tanzania itaweka historia ya kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kumiliki teknolojia hiyo na kutumika katika ligi.

“Huenda VAR ikatumika katika mechi za Ngao ya Jamii, kwa ajili ya kuanza majaribio kabla ya kuanza kutumika kwenye Ligi Kuu. Sehemu kubwa ya kuruhusiwa kwa teknolojia hiyo imekamilika, ila inasubiriwa kutolewa taarifa rasmi na mamlaka husika,” kilisema chanzo kutoka ndani ya TFF.

Chanzo hicho kimedokeza kuwa wataalamu waliopewa mafunzo ya kuitumia teknolojia hiyo wakishirikiana na maofisa wengine ndio watakaosimamia shoo katika majaribio hayo, ingawa TFF inafanya siri kwa sasa.

Tangu taarifa ya kwamba VAR itaanza kutumika katika Ligi Kuu ya msimu ujao, baadhi ya wadau wamekuwa na maoni tofauti, wengine wakiamini itasaidia kupunguza dosari zilizokuwa zikichangia kuitibulia hadhi ya ligi hiyo kwa misimu ya hivi karibuni, na wapo wanaona ilipaswa kuwa viwanja vyote na sio Kwa Mkapa tu.

Kuhusu  ukweli wa jambo hilo, Mwenyekiti wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi alisema atafutwe Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko, Boniface Wambura ambaye simu yake iliita bila kupokewa.

Related Posts