Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesimulia namna Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa alivyomuhamasisha kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kumlipia ada ili kufanikisha jambo hilo.
Dk Nchimbi amesimulia hayo leo Jumapili Julai 28, 2024 alipotembelea kaburi la hayati Mkapa lililopo katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na kushiriki ibada fupi ya kumwombea kiongozi huyo.
Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020 katika Hospitali ya Lugalo iliyopo Dar es Salaam na kuzikwa Julai 29, nyumbani kwake, Lupaso.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kumsikiliza, Dk Nchimbi amesema yeye ni mmoja wa wanafunzi wa kisiasa wa hayati Mkapa na alibahatika kufanya naye kazi kwa miaka saba, akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Mkapa akiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Amesema siku moja akiwa na Mzee Mkapa, alimuuliza kuhusu elimu yake, akamjibu ana shahada ya kwanza pekee. Mkapa alimwambia kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa UVCCM, elimu hiyo haitoshi huku akihoji sababu za kutotaka kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Dk Nchimbi ameeleza alimwambia Mkapa kwamba hakuendelea na masomo kwa sababu alikosa ada, “aliniitikia na mazungumzo yetu yaliishia hapo.
“Nilidhani nikimwambia nimekosa ada mazungumzo yataishia hapo, kumbe Mzee Mkapa aliendelea kufuatilia, alipenda sana niendelee na masomo,” amesema Dk Nchimbi.
Katibu Mkuu huyo amesema siku iliyofuata, alitafutwa na mtu mmoja, akamwambia ana barua yake. Walipoonana akamweleza kwamba: “Rais Mkapa amefuatilia ada za vyuo vikuu vya Mzumbe na Dar es Salaam, hazizidi Sh2 milioni, hizi hapa, kalipie.”
Amesema alikabidhiwa fedha hizo na baada ya kuona Mzee Mkapa anafuatilia, ilimbidi aombe chuo na kuanza masomo ya shahada ya uzamili. “Kabla ya miezi sita kupita Mkapa alinipigia simu kuniuliza shule inaendeleaje.”
“Wewe Rais ametaka ukasome, akakulipia na ada, utakataa kwenda kusoma?” Dk Nchimbi aliwauliza wananchi waliokuwa wakimsikiliza, nao wakamjibu…utakwenda.
Asikitika kutohudhuria maziko yake
Dk Nchimbi ameeleza kitu kikubwa kilichompa shida kwenye nafsi yake ni kutohudhuria mazishi ya kiongozi huyo ambaye alifanya mabadiliko makubwa wakati wa utawala wake yaliyoiletea nchi maendeleo.
“Nakumbuka kipindi hicho kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa corona, viwanja vya ndege vilifungwa, sikuweza kusafiri kabisa. Ndiyo maana niliporudi nchini, nilikwenda moja kwa moja kumpa pole Mama Anna Mkapa.
“Leo nafarijika kufika hapa alipolala. Mzee Mkapa hawezi kusahaulika kwa Watanzania wote, alifanya kazi kubwa ya kuleta mabadiliko katika Taifa hili,” amesema Dk Nchimbi.
Amewahakikishia wananchi kwamba chama chake kitaendelea kuimarisha na kuendeleza kazi kubwa aliyoianzisha Mzee Mkapa.
“Niwapongeze wananchi wa Lupaso kwa kumpa heshima Mzee Mkapa kwa CCM kuendelea kuongoza kata hii. Isingekuwa heshima kata hii kuongozwa na chama kingine tofauti na CCM,” amesema Dk Nchimbi.
Amesisitiza kwamba kipaumbele cha kwanza cha wanaCCM ni utumishi bora kwa Watanzania wenzao.