LITAKUWA ni juma lililosheheni shughuli nyingi kama mzinga wa nyuki kwenye viwanja vya Dar Gymkhana na TPDF Lugalo yatakakofanyika mashindano mawili makubwa ya kuukaribisha mwezi Agosti jijini, Dar es Salaam.
Kwenye viwanja vya TPDF Lugalo, mwezi Agosti utakaribishwa na mashindano ya wazi ya KCB yatakayoshirikisha wachezaji kutoka klabu zote nchini na wachezaji wa jinsi zote wakiwemo watoto, kwa mujibu wa nahodha wa klabu hiyo, Meja Japhet Masai.
Wikiendi ijayo pia, klabu ya Dar Gymkhana na Arusha Gymkhana pia zitakuwa katika pambano wa kukata na shoka ili kujua nani ni mbabe kati ya klabu hizo mbili.
Mashindano ya Gofu ya Lugalo yatapata mshindi kwa kuhesabiwa pointi za viwanjani (stableford point) mashindano ya Inter-Club kati ya Dar Gymkana na Arusha yatashindanisha wachezaji kwa ubora wa mikwaju (stroke-play).
Fred Laizer ambaye ndiye nahodha wa klabu ya Dar Gymkhana alisema mashindano ya Inter-Club ni mfumo wa mashindano ya gofu ambao huzikutanisha klabu mbiIi ambapo wachezaji kutoka klabu moja hushindanishwa na wale wa klabu pinzani na anayeshinda huipa pointi timu yake.
“Tunawakaribisha wote kushiriki kwani ni mashindano yanayoufungua mwezi Agosti,” alisema Mwenyekiti wa Klabu ya Dar es Salaam Gymkhana, Lesse Sayore.
Lengo la michuano ya klabu, kwa mujibu wa Sayore, ni kuboresha mchezo wa gofu, kuleta ushindani na kujenga urafiki.
“Tuna wachezaji wengi wazuri katika klabu yetu ambao nina imani watatuwakilisha vyema dhidi ya wapinzani wetu kutoka Arusha,” alisema Sayore.
Mchuano huo kati ya Arusha Gymkhana na Dar es Salaam, unatarajiwa kufanyika Agosti 3 kwenye viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana.
Mashindano ya mwisho ya Inter-Club yalifanyika mwezi Machi kawenye viwanja vya Lugalo na yalishirikisha klabu tatu za Dar es Salaam Gymkhana, Tanzania People’s Defence Forces (TPDF) Lugalo na Morogoro Gymkhana.
Baada ya Dar Gymkhana kuibuka mbabe, klabu hiyo ina matumaini pia ya kuifunga Arusha zitakapokabiliana jijini Dar es Salaam.