UNAWEZA usiamini, lakini ndio ukweli ulivyo. Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Jhonier Blanco hafai kwa matumizi ya makipa. Hivi ndivyo unavyoweza kusema kumhusu raia huyo wa Colombia.
Hapa sizungumzii mabao ambayo ameshafunga hadi sasa katika mechi za maandalizi kabla ya msimu, hapana. Nazungumzia maajabu anayoendelea kuyaonyesha kambini mjini Benslimane hapa Morocco.
Kwenye mazoezi kuelekea mchezo wa leo wa kirafiki dhidi ya Union Touarga, Blanco alimvunja kidole gumba kipa wa Azam FC, Khamis Yassin aliyepandishwa tangu msimu uliopita kutoka timu za vijana.
Akiwa nje ya 18, Blanco aliachia shuti kali ambalo kipa huyo chipukizi alijitahidi kulizuia na kujikuta matatani.
Papo hapo akaanguka chini na kuanza kulia kwa sauti kali akiomba msaada wa matibabu.
Madaktari wa timu wakafika na kumpa huduma ya kwanza, kisha kumpeleka hospitali alikobainika kidole gumba cha mkono wa kushoto kimeumia na anaweza kukaa nje kwa mwezi mmoja.
Blanco ni mshambuliaji mwenye mwili wa kishambuliaji kwelikweli. Ana nguvu kubwa za miguu na kumfanya awe na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali.
Na hii ni kama tahadhari kwa makipa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao. Inawezekana ikashuhudiwa makipa wengi wakichaniwa glovu au kuumia mikono.
Zaidi ya kuchana glovu au kuvunja mikono ya makipa, yawezekana nyavu nazo zikawa hatarini kama ilivyotokea Kigoma, Novemba Mosi, mwaka jana pale Gibril Sillah alipochana nyavu katika mchezo wa Mashujaa dhidi ya Azam FC uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.
Zamani matukio ya kuchana nyavu na hata kupasua mipira yalikuwa ya kawaida kwa sababu vifaa hivyo vilitumika vikiwa vimechakaa. Ilikuwa ni kawaida kwa uwanja mmoja kuwa na mpira mmoja tu na huohuo ukatamika hapo kwa kila mechi
Na hii ndiyo sababu ya mipira kupasuka wakati ule. Lakini sasa hali haipo namna hiyo. Uwanja mmoja una mipira zaidi ya mitano kwa mechi. Kwa hiyo mpira ukipasuka ni kutokana na mashuti zaidi siyo tu kuchakaa.
Na mmoja wa wachezaji wanaoweza kupasua mipira ni Blanco.
Ila sasa kaanza kuumiza mikono makipa, akianza na kipa wa timu yake.
Azam inaendelea kujifua na usiku wa jana ilikuwa uwanjani kucheza mechi ya pili ya kirafiki hapa Morocco na kesho Jumatatu itamalizia kwa kuvaana na Wydad Casablanca kabla ya kuvunja kambi na kuanza kurudi nyumbani, lakini ikipitia kwanza Kigali, Rwanda kucheza mchezo mwingine wa kirafiki wa kimataifa.
Ikiwa Kigali, Azam itatambulisha kikosi kipya cha msimu ujao kwenye Tamasha la Azamka na kusindikizwa na pambano dhidi ya wenyeji, Rayon Sport, inayonolewa na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyerejea baada ya kupitia Vipers ya Uganda na Simba iliyomtemesha kibarua baada ya kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga katika pambano la Dabi ya Kariakoo lililopigwa Novemba 5, mwaka jana.
Shughuli yote hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali kuanzia saa 10:00 jioni kisha baada ya baada ya hapo Azam itaenda Zanzibar kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Agosti 8 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja.
Jhonier Alfonco Blanco Yus alizaliwa, Oktoba 18, 2000 katika mji wa Santa Marta, Colombia na kuanza kucheza soka mtaani kabla ya kuchukuliwa na Akademi ya Club Depotive, kisha akaenda kujiunga na timu ya vijana U20 ya Aguilas Doradas hadi mwaka 2021 alipotua klabu ya Rionegro Aguila iliyopo Ligi Kuu (Categoria Primera A) ambayo Januari mwaka jana ilimtoa kwa mkopo kwa Fortaleza CEIF.
Akiwa na timu hiyo ya Daraja la Kwanza (Categoria Primera B) alipoibuka Mfungaji Bora akifunga mabao 15 na kuipandisha timu daraja na kuchukua ubingwa wa ligi hiyo. Lakini alihitimisha msimu huo kwa rekodi nzuri ya kufunga jumla ya mabao 18 katika mechi 26 alizocheza katika mashindano yote.
Alipomaliza mkopo alirejea klabu ya Rionegro hadi Julai Mosi aliponunuliwa na Azam FC na katika mechi mbili ambazo Azam imecheza hadi sasa za kirafiki (kabla ya mechi jana), Blanco ameshafunga mabao matatu, mawili akiitungua Zimamoto iliyolazwa mabao 4-0 na moja alitupia wakati wakiizamisha US Yacoub Mansour kwa mabao 3-0.
Blanco ni mchezaji anayetumia zaidi mguu wa kulia, lakini akiwa ni mahiri kwa kupiga mashuti akitumia miguu yote, na ni mzuri kwa mipira ya vichwa mbali na uwezo wa kumiliki mpira na kupiga chenga.
Kwa kile alichoonyesha hadi sasa ni wazi makipa wa timu pinzani wana kazi ya kujiweka sawa kabla ya msimu mpya kuzinduliwa Agosti 8 na kuanza kwa Ligi Kuu Bara, Agosti 16.