WIKI tatu ambazo KenGold imekaa katika mji wa Tukuyu ikijifua kwa ajili ya Ligi Kuu, zimewafanya vijana wa timu hiyo kuwa tayari kuingia uwanjani japokuwa kwa sasa kocha mkuu wa KenGold, Fikiri Elias amesema anatafuta kikosi cha kuanza (First Eleven).
Msimu ujao unaoanza Agosti 16 ndio wa kwanza kushiriki Ligi Kuu kwa timu hiyo iliyopanda daraja ikiendelea na kambi yake huko Tukuyu na wiki hii itaanza kushiriki mashindano ya Mbeya Pre-Season ambayo hufanyika kila mwaka wilayani Kyela.
Elias aliliambia Mwanaspoti kuwa kambi waliyonayo huko Tukuyu inampa hamasa kubwa kutamba kufanya vizuri kutokana na kile wanachoonyesha mastaa ikiwamo kasi na utimamu.
Alisema pamoja na muunganiko anaoendelea kuutengeneza, anaumiza kichwa kupata kikosi cha kuanza (First Eleven) pale ligi itakapoanza ili kuhakikisha wanapoingia uwanjani wafanye kweli.
“Vijana wanaonyesha uimara, utimamu na utayari, benchi la ufundi tunasuka muunganiko kila mara ila bado sijapata wale 11 wanaoweza kuanza, hii ni kwa kuwa tumechanganya wachezaji,” alisema Elias.
Kocha huyo wa zamani wa Coastal Union, aliongeza kuwa licha ya timu kuwa mwishoni kukamilisha usajili lakini anao uhitaji wa beki mzoefu kuimarisha sehemu ya ulinzi na kutengeneza ukuta utakaokuwa imara.
Alisema baada ya siku 21 kambini huko Tukuyu, mapema wiki hii wataanza kushiriki mashindano ya Mbeya Pre-Season ambayo yatatoa mwanga na nafasi kwa benchi la ufundi kubaini ubora na udhaifu wa timu.
“Tutatumia mashindano hayo kama moja ya kupima wachezaji kuona ubora na udhaifu wao kabla ya kuanza ligi, kimsingi tunaendelea kujipanga vyema na matarajio ni kufanya vizuri, tunasubiri tu siku ifike,” alisema kocha huyo.