Ifakara. Matukio ya watu kuvamia na kutenda mambo yasiyoruhusiwa katika nyumba za ibada yameendelea kujitokeza baada ya Enock Masala (19), mkazi wa Ifakara, mkoani Morogoro kujikuta matatani alipotaka kutoroka na ekaristi takatifu.
Hata hivyo, katika maelezo yake, Masala amedai kuwa yeye si mkatoliki na alitenda tukio hilo baada ya kuona wakristo wengine wakipanga foleni na kupokea ekaristi takatifu.
Amedai hakuwa anajua kama ni kosa kuondoka na ekaristi takatifu na hakujua kama inachukuliwa mara moja na hajui taratibu za kanisa hilo.
Alipoulizwa kwa nini alikwenda kwenye ibada katika kanisa hilo ilhali si mkatoliki, kijana huyo hakuwa na majibu.
Tukio hilo limetokea leo Jumapili, Julai 28, 2024 wakati wa misa ya kwanza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea Jimbo Katoliki Ifakara, baada ya kijana huyo kukominika, alimua kuificha ekaristi takatifu na kuondoka nayo bila kuitia mdomoni.
Hata hivyo, Masala hakufanikiwa kuondoka na ekaristi takatifu kwa kuwa alijikuta akiingia mikononi mwa walinzi wa kanisa hilo, huku Paroko wa kanisa hilo, Marcus Mirwatu akilaani kitendo hicho.
Amesema kumekuwa na wimbi la matukio ya watu wasio wakatoliki kuingia kanisani kukomunika, kisha kuondoka na ekaristi takatifu.
Matukio kama hayo kwenye nyumba za ibada yamekuwa yakitokea, wapo wanaoingiza nyumba za ibada na kuiba vifaa fedha, mikeka, vyombo vya muziki, ekaristi takatifu na kufanya uharibifu mwingine.
Baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Padre Mirwatu amesema mpaka sasa bado kanisa halijafahamu nia ya watu wasiokuwa wakatoliki kuingia kanisani na kuondoka na sakramenti, hata hivyo kanisa limeanza kuimarisha ulinzi wakati wote wa ibada.
Kiongozi huyo wa kanisa amelaani vitendo hivyo na kuaziga wakristo kuwafichua watu hao, wanaokwenda kinyume na imani ya kanisa hilo, huku akiwataka walinzi kuwa makini wakati wa ibada.
“Tunashindwa kuelewa watu hawa wanatumwa na nani kufanya vitendo hivi, hatuelewi wana malengo gani kwa kanisa letu, hivyo ninaomba kijana huyu aendelee kuhojiwa kwa nini amefanya tukio hilo,” amesema Padri Mirwatu.
Kijana huyo ameendelea kuwa chini ya ulinzi, jitihada za kulipata Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kujua kama wamekwenda kumchukua zinaendelea.