Kiuno chako kimezidi inchi hizi, upo hatarini kupata tatizo la kiafya

Namtumbo. Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohammed Janabi amesema kuwa iwapo mwanaume mzunguko wa kiuno chake utazidi 40 (inchi) na mwanamke ukizidi  35 kitakuwa ni kiashiria cha matatizo ya kiafya.

Profesa Janabi amesema kuwa iwapo viuno vitazidi inchi hizo ni changamoto, maana yake ana uzito mkubwa ambao unawaweka kwenye hatari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Janabi ameyasema hayo leo  Julai 28, 2024 wakati akizungumza na mamia ya wananchi  wa Kijiji cha Mtakanini, Wilaya ya Namtumbo ambao walijitokeza kwenye Kituo cha Afya Mtakanini kufanyiwa uchunguzi na kutibiwa bure kwenye kambi ya madaktari  bingwa iliyoanza Julai 24 hadi Julai  28 mwaka huu.

Kambi hiyo ilikuwa ikiangazia magonjwa mbalimbali yakiwemo ya saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, saratani ya matiti, tezi dume, kisukari pamoja na homoni.

Profesa Janabi amesema kama ambavyo pombe haijawahi kumuacha mtu salama na kitambi vivyo hivyo.

“Naomba mjitokeze kupimwa viuno vyenu, maana kama kuna mwanaume ana kiuno cha zaidi ya inchi 40 hiyo ni changamoto, kama kuna mwanamke ana mzunguko wa kiuno wa zaidi ya inchi 35 pia ni changamoto. Maana uzito ni mkubwa na anaweza pata magonjwa yasiyoambukiza hivyo aje kutibiwa na madaktari msiwachaji fedha nyingi,” amesema Profesa Janabi.

Akizungumza kuhusu saratani ya shingo ya kizazi, Profesa Janabi amesema inaongoza kusumbua akina mama wengi ambao wanatibiwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), hivyo amewataka kuacha kusikiliza uvumi kuhusu namna ya kupimwa saratani  ya shingo ya kizazi na tezi dume.

Badala yake amewataka wajitokeze kupima na kuacha kusikiliza maneno ya mitandaoni kwani saratani  hizo zipo na zinaua na wasisubiri hadi isambae zaidi.

Amesema, saratani  ya tezi dume  inakua taratibu na inachukua miaka 15 hadi 20 kujitokeza, “hivyo vijana  wanaosema  tezi dume  ni ugonjwa wa wazee  si kweli.

Amesema vijana wenye miaka 30 nao  wajitokeze kupima kipimo cha tezi dume  mara moja kwa mwaka kwani, inakua taratibu hivyo wasiogope wajitokeze kuchunguzwa ili wapate uhakika kuliko kuiachia ianze kuwatesa wakiwa na miaka 50.

“Akina Baba kipimo kile kisiwatishe jitokezeni kupima tezi dume ili mjue afya zenu na kutibiwa mapema, msiogope kile kipimo kingine kwani tunaanza na kipimo cha damu kwanza na kisha inatupa viashiria kama unayo tunaanza kukupatia matibabu kabla haijasambaa kwenye uti wa mgongo na mapafu,” amesema Profesa Janabi.

Awali akitoa taarifa fupi ya kambi hiyo, kiongozi wa timu ya madaktari bingwa wanne toka MNH, Dk Joachim Angelo amesema hadi jana wamehudumia wagonjwa 232 ambapo miongoni mwao wanawake ni 184.

Amesema, jumla ya wanawake 66 wamehudumiwa kwa kufanyiwa vipimo vya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti, maambukizi kwenye via vya uzazi pamoja na matatizo ya ugumba na hedhi ambapo akina mama 18 wamekutwa na tatizo.

Aidha, amesema pamoja na mafanikio hayo wamebaini changamoto za ukosefu wa baadhi ya dawa muhimu, kukosekana vipimo vya msingi FBP kwa upande wa maabara na huduma ya X-Ray.

Mbunge wa  Namtumbo, Vita Kawawa amemshukuru Profesa Janabi  kwa kutoa elimu kwa wananchi wa eneo hilo, dawa za magonjwa mbalimbali ambazo zimegawiwa bure, mashine ya kupima sukari na vitabu 100 vya mtindo wa maisha  na afya.

Naye mkazi wa kijiji hicho, Hawa Athuman amesema matibabu na elimu aliyopata yamemsaidia kutambua changamoto aliyonayo ya shingo ya kizazi.

Mganga Mfawidhi  kituo cha Afya Mtakanini, Dk John Nyagana amesema ujio wa madaktari  bingwa toka Muhimbili umesaidia wananchi kupata huduma ya matibabu ya mfumo wa mkojo, saratani ya shingo ya kizazi, sukari na homoni.

Amezitaja changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho kuwa ni kutokuwepo kwa wodi ya kulaza wagonjwa wa jumla, hivyo kulazimika kutumia vyumba vya mapumziko vya muda kwa ajili hiyo.

Related Posts