Sera ya Taifa ya Biashara kuzinduliwa Tanzania, kufungua fursa

Dar es Salaam. Serikali inatarajia kuzindua Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2023 inayolenga kuondoa vikwazo vilivyokuwapo awali na kuboresha mazingira, ili kuchochea ufanyaji biashara ndani na nje ya nchi.

Pia, sera hiyo inalenga kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika pato la Taifa, kuchochea ajira na uwezo wa bidhaa za Tanzania kuyafikia masoko yaliyopo ya Bara la Afrika.

Sera hiyo ya mwaka 2023 inayotarajiwa kuzinduliwa Julai 30, 2024 jijini Dar es Salaam ina maboresho yanayolenga kuziba pengo lililokuwa limeachwa, huku ikibebwa na kauli mbiu isemayo:”Ushindani wa biashara katika kuchochea kasi ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayoongozwa na viwanda.”

Akizungumza leo Jumapili, Julai 28, 2024, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema wanategemea kuzinduliwa kwa sera hiyo kutaongeza mchango wa sekta ya biashara katika pato la Taifa.

“Pia, itasaidia kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini na kuvutia uwekezaji, kuongezeka kwa shughuli za biashara, ajira na kuongezeka kwa kipato cha wananchi,” amesema Dk Jafo.

Pia, amesema sera hiyo itasaidia kuongezeka kwa uzalishaji viwandani kutokana na upatikanaji wa masoko ya uhakika, hivyo kuchochea jitihada za ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Pia, imeelezwa sera hiyo itachochea kuwepo kwa ushindani huru na haki katika biashara na kumlinda mlaji, kuimarika kwa uratibu wa biashara na kuondokana na mgongano wa kisera, kisheria na mgawanyo wa majukumu ya kitaasisi katika masuala ya biashara.

Pia, amesema itasaidia kuimarika kwa miundombinu ya masoko na biashara.

Hadi uamuzi huo unafikiwa, uchambuzi uliofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara ulibainisha changamoto zilizokuwa zikiathiri utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003.

Changamoto hizo ni uwezo wa sekta binafsi kutumia fursa za biashara, mazingira magumu ya kisheria, teknolojia duni na uwiano mdogo wa Sera ya Biashara.

 Pia, zilikuwapo changamoto za kimazingira kama mabadiliko ya hali ya hewa, ujuzi mdogo katika masuala ya biashara na urasimishaji mdogo wa biashara, miundombinu duni, vikwazo vya kibiashara hasa vya kiushuru na mgongano wa majukumu ya taasisi.

“Hivyo, uchambuzi huo, ulithibitisha haja ya kuifanyia marekebisho Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 na kuandaa mkakati wake wa utekelezaji, ili kukidhi mahitaji na matakwa ya sasa na ya baadaye,” amesema Dk Jafo.

Amesema mbali na kuonekana kwa changamoto zilizochochea mapitio hayo, lakini sera ya mwaka 2003, iliisaidia Tanzania kushiriki kikamilifu katika majadiliano mbalimbali ya biashara baina ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa na kuongeza fursa zaidi za biashara ya bidhaa na huduma kutoka Tanzania.

Hiyo ilijumuisha kupatikana kwa masoko yenye masharti nafuu kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania, likiwamo soko la Afrika ya Masharikia (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Pia, sera hiyo ilisaidia kupatikana kwa soko la China la kuuza bidhaa bila kulipa ushuru wala kikomo kwa asilimia 98 ya bidhaa zote kutoka Tanzania, India, soko la Agoa la kuuza bidhaa 6,400 bila ushuru Umoja wa Ulaya.

“Kwa jumla, kukua huku kwa biashara kumewezesha mchango wa biashara katika Pato la Taifa kufikia asilimia 8.3 mwaka 2023.

Kupitia fursa hizo mauzo kwenda Jumuiya ya Afrika Mashariki yameongezeka kutoka Sh1.12 trilioni mwaka 2016 hadi Sh3 trilioni mwaka 2023,” amesema Dk Jafo.

Amesema pia sera hiyo ilichochea kuongezeka kwa mauzo nje kwenye jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika kutoka Sh2.6 trilioni mwaka 2016 hadi Sh4.4 trilioni mwaka 2023.

Mauzo kwenye Jumuiya ya Ulaya kutoka Sh0.6 trilioni mwaka 2016 hadi Sh3.8 trilioni mwaka 2023.

“Bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni pamoja na bidhaa za kilimo, hususani kahawa, chai, mahindi, ngano, mchele na  mbogamboga,” amesema Dk Jafo.

Mkurugenzi wa Trade Mark Afrika (TMA), Elibariki Shammy amesema mapitio ya sera hiyo yamechukua kati ya miaka mitatu hado minne linaloonyesha dhamira nzuri ya kuboresha biashara nchini.

Amesema kiu ya TMA ni kuona nchi nyingi za Afrika zinafanya kile kilichofanyika Tanzania kwa kuwa sera za biashara ndiyo zimekuwa kipingamizi kikubwa cha kukwamisha biashara za kikanda.

“Tunasaidia nchi nyingi za Afrika kwa lengo la kupunguza gharama na muda wa kufanya biashara ndani ya Bara la Afrika, lakini bado nchi na nchi haziwezi kufanya biashara kwa sababu sera na taratibu zinakinzana na gharama za kufanya biashara kati ya nchi moja na nyingine zinakuwa bei ya juu,”  amesema Shammy.

Amesema gharama za ufanyaji wa biashara zinatokana na yale yanayofanyika katika biashara ya ndani, hivyo sera hiyo kuzungumzia namna ya kutatua changamoto zilizokuwapo ni jambo jema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts