Serikali kuja na mbinu mpya kukabili utekaji watoto

Dar es Salaam. Wakati kukidaiwa kuwepo kwa vitendo vya utekaji dhidi ya watoto nchini Tanzania, Serikali imefanya maboresho ya mifumo na mikakati ya kuyakabili.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, licha ya kuwepo kwa matukio hayo, yanavyoripotiwa ni tofauti na uhalisia wa wingi wake.

Kauli hiyo ya Serikali inakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na taharuki inayosabababishwa na madai ya kukithiri kwa vitendo vya utekaji dhidi ya watoto.

Masauni amesema hayo leo Jumapili, Julai 28, 2024 katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika ofisi ndogo za wizara hiyo, jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa matukio ya kihalifu mwa mwezi Julai.

Waziri huyo ametoa mikakati hiyo mbele ya waandishi akitanguliwa na kikao cha ndani kilichohusisha taasisi zilizo chini yake, akiwemo naibu wake, Daniel Sillo na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura.

Kikao hicho kinafanyika ikiwa zimepita siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuwaomba machifu na viongozi wa mila kukemea vitendo hivyo katika ngazi za chini wanakotoka.

Rais Samia alieleza hayo Julai 20, 2024 alipokutana na machifu wote nchini, Ikulu ya Chamwino, Dodoma akisema mauaji ya watu wenye ualbino na utekaji yameibuka upya na yanaichafua Tanzania.

Alisema kumekuwa na matukio hayo ambayo wakati mwingine si ya kweli na lawama zinaelekezwa serikalini na pengine vyombo vya ulinzi na usalama.

“Hii sio Tanzania tunayoitaka, niwaombe machifu wenzangu, tulinde watoto wetu, tulinde kutumia mila na desturi zetu,” amesema.

Katika maelezo yake, Waziri Masauni amesema Serikali inatambua kuwepo kwa matukio hayo, ingawa si kwa ukubwa kama inavyoripotiwa.

“Siwezi kukaa mbele yenu nikasema eti hakuna matukio ya ubakaji na ukatili wa watoto, nadhani nitakuwa muongo kupitiliza na pengine sitapaswa hata kuwepo hapa mbele.

“Uhalifu katika nchi yetu upo, ulikuwepo na utaendelea kuwepo kwa sababu binadamu hatujaumbwa kufikiria sawa, isipokuwa tunaunda mkakati na kutafuta mbinu za kupambana nao,” amesema.

Kutokana na uhalisia huo, amesema kinachofanywa sasa ni kuboresha mifumo na taratibu za kukabili vitendo hivyo na sio kutumia mbinu za kale.

Ameeleza uboreshaji huo, unahusisha kuja na mbinu mpya na za kisasa zitakazoendana na wakati uliopo.

Sambamba na hilo, amesema kwa ujumla matukio ya uhalifu yamepungua, akitaja kwa asilimia tano.

Hata hivyo, amesema anakiri kuwepo kwa matukio ya kihalifu na Serikali inaendelea kuchukua hatua.

Akirejea baadhi ya matukio, Masauni amesema Julai 12, mwaka huu Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam mtoto mmoja alitoweka na baadaye kukutwa amebakwa na tayari mtuhumiwa ameshakamatwa.

Julai 12, mtoto alipotea Oysterbay, Dar es Salaam na Julai 15 walimkuta Mikumi na alichukuliwa na msichana wa kazi na waliofanikisha ni wazazi wa msichana wa kazi.

Julai 22 mkoani Geita, amesema mwanamama anayedaiwa kumuua mwanawe mmoja kati ya wawili aliowazaa amebainika na kukamatwa.

Kadhalika, amesema wilayani Chalinze, Mkoa wa Pwani, Mwalimu wa Shule ya Msingi Vigwaza na watu wengine watatu wanashikiliwa kwa kutoa taarifa za uzushi wa kutekwa na kuchinjwa kwa watoto katika shule hiyo.

Amesema sambamba na kudhibiti wahalifu wa matukio hayo, pia watawakabili wale wote wanaosambaza taarifa za uongo kuleta taharuki.

“Kuna mazingira watu wanatumia changamoto ya uhalifu badala ya kushikamana, watu wanatumia kwa faida zao binafsi kutaka kuuza kwenye vyombo vyao, kisiasa au kuleta taharuki tu,” amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts