Serikali Nigeria ‘yawapitia denge’ waandamanaji, yatangaza ajira

Lagos. Wakati kukiwa na fukuto la vijana wa Nigeria kuandamana wakidai utawala mbovu na gharama za maisha kuwa juu, Serikali ya nchi hiyo imewawahi kwa kuwatangazia ajira.

Hatua ya Serikali ya nchi hiyo kutangaza ajira kwa vijana katika kampuni yake ya mafuta  pamoja na ruzuku ya mabilioni ya Naira imekuja kama hatua ya kuzima maandamano hayo.

Reuters imesema wanaharakati wa Nigeria wanajaribu kuiga maandamano yanayoongozwa na vijana kwingineko barani Afrika, ambayo yametikisa Serikali ikiwemo ya nchini Kenya huku vuguvugu kama hilo likihamia Uganda.

Kampuni ya mafuta ya Serikali ya Nigeria, juzi Ijumaa imechapisha nafasi za kazi za nchi nzima katika chapisho kwenye X (zamani Twitter) kwa mara ya kwanza ikiwa haijafanya hivyo kwa takriban muongo mmoja.

Msemaji wa kampuni ya NNPC Ltd, iliyotangaza ajira hizo, Olufemi Soneye amesema maombi yamekuwa mengi kiasi cha kuiharibu tovuti ya kampuni hiyo.

Ijumaa iliyopita pia  Wizara ya Maendeleo ya Vijana ya Nigeria ilizindua mfuko wa uwekezaji kwa vijana wa Naira bilioni 110 ambazo ni sawa na Dola za Marekani milioni 70 (zaidi ya Sh188 bilioni) unaolenga kutoa ruzuku kwa vijana wa nchi hiyo ili kuzalisha ajira.

Hata hivyo raia wa nchi hiyo kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakipanga maandamano ya nchi nzima wiki ijayo kupinga kupanda kwa gharama za maisha ambapo kumesababisha  mfumuko wa bei kupanda kutoka asilimia 28 hadi kufikia asilimia 34.2.

Reuters imesema hiyo inakuja kufuatia kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta na kushuka kwa thamani ya sarafu.

Hata hivyo, viongozi wa kidini, watawala wa kitamaduni na Wanigeria na watu mashuhuri wameungana na Serikali kuwakatisha tamaa vijana kufanya maandamano yanayotarajiwa kuanza Agosti 1,2024 wakihofia yataharibu uchumi.

Kwa upande mwingine viongozi wa polisi na jeshi wa nchi hiyo wameonya hatua hiyo, huku waandamanaji wakisema wana haki ya kufanya maandamano ya amani.

Related Posts