Dar es Salaam. Dunia imebadilika, jamii pia imetoka kwenye msingi wa malezi, jambo linalosababisha watoto wengi kutokuwa salama katika makuzi yao.
Japo kuna maeneo ni jambo la kawaida kumkuta mtoto akicheza katika mazingira ambayo si rafiki kwa umri wake, mzazi hajali na kuchukulia ni kawaida, jambo ambalo linatajwa kuwa kichocheo cha ukatili dhidi yao.
Mchambuzi wa masuala ya malezi ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Christian Bwaya anasema ulinzi wa watoto unaanza na wazazi.
Anasema, nyakati hizi usalama wao unaonekana kupungua kutokana na maisha na dunia kubadilika, huku wazazi wengi wakishindwa kufuata misingi ya malezi.
“Zamani tukiwa watoto tulikuwa tunacheza tu kwa kuwa mazingira yalituruhusu kufanya hivyo na kulikuwa salama kwa watoto kucheza, tofauti na nyakati hizi,” anasema Bwaya.
Anasema nyakati hizi mtoto anapokwenda kucheza mzazi anawajibu wa kufahamu anacheza wapi na nani na wanacheza nini? Kwani kuna matukio mengi ya kikatili watoto wanafanyiwa hadi na watoto wenzao, ukiachaana na haya ya kutekwa.
Bwaya anasema wazazi wengi kutokana na hali ya maisha na changamoto za kiuchumi, wanajikuta wakitumia muda mwingi kutafuta fedha.
Hii inasababisha wawe na muda mchache wa kuwa na watoto wao, kufahamu changamoto wanazokutana nazo na kushirikiana nao katika kuzitatua. Hali hii inaweza kuathiri ukuaji na maendeleo ya kihisia na kijamii ya watoto.
“Tunahitaji kurudi kwenye msingi wa malezi, mzazi kufuatilia ratiba ya mtoto wake ni jambo la muhimu, kumwekea ratiba ya muda wa kucheza, acheze katika mazingira gani na acheze kitu gani, hili ni jambo jingine la muhimu katika malezi,” anasema Bwaya.
Hata kama mzazi yuko bize, ni muhimu kutenga japo dakika 15 kwa siku za kuzungumza na mtoto wake, kwa sababu hii itamsaidia kufahamu mengi anayopitia.
Anasema, mambo ya kuzingatia unapozungumza na mtoto ni pamoja na kumpa mbinu za kujilinda. Aelezwe madhara ya kuwa nje ya mazingira ya kwao akicheza peke yake kwamba ni hatari kiasi gani, tofauti na akiwa na wenzake, na ikitokea akaitwa na mtu asiyemfahamu asikubali.
“Mtoto apate mbinu za kujilinda, aelezwe madhara ya kuwa nje ya mazingira ya kwao akicheza peke yake hatari ni kiasi gani, tofauti na akiwa na wenzake na ikitokea akaitwa na mtu asiyemfahamu asikubali.
“Ukimpa elimu hiyo mtoto unamuongezea usalama wake, wakati mwingine wao hawaelewi, akimuona mtu mkubwa amemuita yeye atafuata tu, lakini anapoelimishwa kuhusu usalama wake inamsaidia,” anasema.
Bwaya anasema, wazazi wengi wanawekeza nguvu kubwa na muda mwingi kwenye shughuli za uzalishaji na nyingine ambazo wanaona kwao ndizo za muhimu na kukosa muda wa kufahamu changamoto za watoto wao.
“Wengine wanaishi mbali na familia zao, na huwa wanachukulia hilo ni jambo la kawaida, hawaioni kama ni changamoto, hali hii inasababisha mtoto aishi bila uangalizi wa karibu, jambo linalomuweka kwenye hatari ya matukio ya kufanyiwa ukatili.
Anasema nyakati hizi kuna changamoto ya baadhi ya watu kuanza kutumia mbinu zisizofaa, wakiamini watapata utajiri kwa kujiingiza kwenye imani za kishirikina, jambo ambalo si sahihi, halifai na linapaswa kukemewa kwa nguvu.
Pia, kuna wanawake ambao shinikizo lao ni kuwa na watoto, anapoona hajapata anahisi akiiba anakuwa amefikia malengo, jambo ambalo si sahihi.
Nasra Rajab anaishi kwa majuto hadi leo, baada ya kuchelewa kugundua mwanaye anafanyiwa ukatili na baba mkwe wake ambaye ni babu mzaa baba kwa binti yake.
“Mwanangu alikuwa akilelewa na bibi yake ambaye pale nyumbani aliishi na mdogo wake (babu), alikuwa darasa la nne, ndipo alianza kufanyiwa ukatili, kwa kuwa sikuwa napata muda wa kuzungumza naye nilikuja kufahamu akiwa darasa la sita tayari kaisha haribikiwa,” anasimulia Nasra.
Anasema hadi leo anajutia kutokuwa karibu na binti yake huyo ambaye hatarajii kama atahitimu darasa la saba mwaka huu kwa sababu ameshaharibikiwa.
Janeth Wilson wa Kibaha Madafu yeye anaamini katika kuwafungia ndani watoto wake, mmoja wa darasa la tano na mwingine wa darasa la tatu, akisema kwa kufanya hivyo watakuwa salama.
“Kama hawaendi shule, naacha nimewapikia kabisa, nawaambia marufuku kutoka nje, siku za shule siwaruhusu waende peke yao, ninahakikisha wana mtu mkubwa anayewapeleka, nafanya hivyo ili kuimarisha tu usalama wao.”
Wakati hao wakifanya hivyo, wapo wale wanaowaachia watoto wao wakacheze na kurudi nyumbani muda wowote watakao, kama ilivyo kwa Ester Makunga, mkazi wa Mbweni.
“Nashukuru hawajawahi kupata madhara, wapo wawili, mmoja wa la kwanza na mwingine wa la nne, lakini kwa hali ilivyo sasa inabidi niwe makini nao zaidi,” anasema Ester.
Hata hivyo, wataalamu wa malezi wanasemajambo hilo si rafiki kwa watoto.
Bwaya anasema jamii inapaswa kurudi kwenye misingi ya familia, wazazi watambue wakijikita zaidi kwenye kutafuta pesa na kusahau wanapolea mtoto wanatengeneza kesho ya familia zao.
“Tukiwekeza kwenye kuthamini na kulea familia, wazazi wakawa karibu na watoto itasaidia kuwaondoa kwenye hatari ya kufanyiwa ukatili, vilevile tukubaliane na ukweli kwamba dunia imebadilika.
Zamani wanafunzi tuliweza kutembea kwenda shule bila tatizo, lakini sasa mambo yamebadilika, tukisema tuwape uhuru watoto kama enzi hizo, itawaweka watoto kwenye wakati mgumu, tulivyoishi sisi sivyo watakavyoishi watoto wetu,” anasema.
Anasema kuna haja ya kufahamu mwenendo wa mtoto kuanzia anapotoka nyumbani kwenda shuleni, japo kuna jamii inaona kufanya hivyo ni kumdekeza mtoto, lakini ili awe salama uangalizi huo ni muhimu.
“Anapotoka shuleni pia kuna haja ya kuweka utaratibu wa kupokelewa, japo sio rahisi kwa mzazi ambaye ana mambo mengi, si vibaya kuweka mtu unayemwamini ambaye atakuwa na jukumu la kuhakikisha mtoto anakwenda shuleni salama na kurudi salama,” anasema.
Anasema kwa shule binafsi nyingi zina usafiri wa kumchukua na kumrejesha mtoto nyumbani, hivyo kuhakikisha amekwenda na kurudi salama, kwa shule ambazo hazina utaratibu huo, zihakikishe watoto wanakuwa salama.
“Wale wanaokwenda shuleni kwa kutembea na kuna watoto eneo hilo hilo ni majirani, basi wahamasishwe kutembea pamoja ili kuwaepusha na hatari ya barabarani,” anasema.
Anasema jamii pia inapaswa kuelimishwa kuhusu njia sahihi ya kutafuta pesa kwa kufanya kazi halali na si kuwaumiza wengine ili upate pesa, hakuna utajiri wa aina hiyo.”
Mwalimu wa malezi wa Shule ya Msingi Juhudi ya Dar es Salaam, Frola Masinde anasema wazazi wanapokuwa wanapambana kutafuta fedha, hawapaswi kusahau jukumu la malezi.
Anasema ni muhimu wazazi kutenga muda wa kuwa karibu na watoto kila siku, kufahamu mahitaji yao, changamoto gani wanazipitia na tahadhari zao ambazo zitawasaidia kujua nini wafanye ili kuwaweka salama.
“Kuzungumza na mtoto ni muhimu na kunamjenga hadi kisaikolojia, kwa sababu kuna umri fulani mtoto anahitaji kuwa na watu wanaomsikiliza ambao kwa umri wa utoto, watu wake muhimu ni wazazi,” anasema Masinde.
Mwalimu mwingine wa malezi wa Shule ya Msingi Filbert Bayi, Teddy Solo anasema wazazi wengi wanashindwa kutofautisha malezi na huduma kwa watoto wao.
“Wanafikiri kulipa ada au kumpeleka mtoto beach ndiyo malezi, hapana, hizo ni huduma ambazo ni wajibu wake kumpatia mtoto, kuna jukumu la malezi pia ambalo wengi wao siku hizi wanaliacha lifanywe shuleni, haipaswi, mzazi akumbuke mtoto huyo hakumzalia mwalimu, yupo pale kumsaidia mzazi kumkuza mwanaye kielimu, hivyo kusaidia katika malezi kwa mtoto huyo ni jambo la msingi,” anasema mwalimu Solo.