Wagombea urais TLS ‘wanyukana’ kwa dakika 150

Dar es Salaam. Suala la kupatikana kwa Katiba mpya, ulinzi wa rasilimali za Taifa na matukio ya utekaji, ni miongoni mwa mambo yaliyojenga msingi wa hoja za wagombea wa urais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), zilizochukua dakika 150 sawa na saa 2:30.

Hoja hizo zilikuwa mithiri ya turufu kwa kila mgombea alipojibu maswali yaliyoulizwa katika mdahalo uliohusisha wagombea wote sita wa nafasi hiyo ya kuwaongoza mawakili kwa miaka mitatu ijayo.

Kati ya majibu ya wagombea hao kuhusu mambo hayo, wapo walioonyesha mikakati ya kupata ufumbuzi wake, huku mmoja akijitenganisha nayo kwa kile alichoeleza hana sababu ya kuwadanganya wapigakura kwa kuwa si jukumu la rais wa TLS kuyasimamia hayo.

Mdahalo huo uliwahusisha mawakili sita wanaowania wadhifa huo kumrithi Harold Sungusia anayemaliza muda wake ambao ni Sweetbert Nkuba, Revocatus Kuuli, Boniface Mwabukusi, Paul Kaunda, Ibrahim Bendera na Emmanuel Muga.

Mengi yaliunogesha mdahalo huo, lakini unasaba wa Wakili Nkuba na Chama cha Mapinduzi (CCM), ulijenga maswali mengi dhidi yake na katika majibu aliweka wazi dhamira ya kuwania nafasi hiyo ni kuwawakilisha mawakili na sio CCM.

Alikwenda mbali zaidi na kueleza, kila mgombea wa nafasi hiyo ana chama chake cha siasa na ni haki ya kikatiba, kwa sababu urais wa TLS ni kwa masilahi ya mawakili.

Amesema haoni uanachama wake wa CCM ukiathiri utendaji atakapokuwa rais wa mawakili.

Wagombea wote sita watapima nguvu ya sera na ushawishi wao kwa mawakili wenzao Agosti 2, 2024, jijini Dodoma, siku itakayofanyika uchaguzi.

Mkutano mkuu wa chama hicho utafunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Huo ni muhtasari wa machache kati ya mengi yaliyojiri usiku wa jana Jumamosi, Julai 27, 2024 katika mdahalo wa wagombea urais wa TLS, uliorushwa mubashara na kituo cha runinga cha Star Tv kupitia kipindi cha Medani za Siasa.

Mdahalo huo uliofanyikia ukumbi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ulioanza saa 3:30 hadi 6:00 usiku. Ni sawa saa 2:30 au dakika 150, wagombea wakiwa wima.

Katiba, utekaji, rasilimali

Ahadi ya Bendera atakapopewa ridhaa ya kuwa rais wa chama hicho kuhusu Katiba, ni kuishauri Serikali ihakikishe inafanya marekebisho katika kasoro zilizopo.

Amezitaja baadhi ya kasoro hizo ni katika usimamizi wa haki za binadamu, ikiwamo ya kuandamana na kukusanyika, kwa maoni yake haoni sababu ya kuombewa kibali kwa polisi.

“Hakuna sababu ya kuomba kibali cha kuandamana polisi. Na nguvu ya polisi katika kumtuhumu mtu iondolewe, haya ni mambo nitakayoishauri Serikali,” amesema Bendera.

Mambo mengine, amesema ni utolewaji wa dhamana uwe chini ya mamlaka ya Mahakama na si polisi au mtu yeyote.

Kuhusu matukio ya utekaji, pamoja na kuonyesha kukerwa nayo, Bendera  amesisitiza atakapokuwa rais ataishauri Serikali kuweka mazingira ya upatikanaji haraka wa taarifa za vitendo hivyo.

Msingi wa swali hilo lililoelekezwa kwa wagombea wote ni uwepo wa madai ya watu kutekwa au kupotea katika mazingira tatanishi na kuwaacha ndugu, jamaa na marafiki wakiwa hawana la kufanya.

Taarifa za matukio hayo zimekuwa zikitolewa na ndugu zao kwa mamlaka. Katika ziara za aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Simiyu, Mwanza ziliibuka taarifa hizo.

Miongoni mwa watu ambao tangu kupotea kwao miaka mitano nyuma haijulikani walipo ni mwanasiasa Ben Saanane na mwanahabari Azory Gwanda.

Katika ulinzi wa rasilimali za Taifa, Bendera amesema atashirikiana na baraza la uongozi la TLS kuishauri Serikali kusimamia hilo na ikishindikana watatumia vyombo vinavyostahili, ikiwamo kwenda mahakamani.

Ahadi ya Paul Kaunda haikupishana sana na Bendera kuhusu kupatikana kwa Katiba mpya, isipokuwa aliahidi kuishauri Serikali iendelee pale ilipoishia katika rasimu ya Katiba ya mwaka 2014.

Rasimu inayozungumzwa na Kaunda ni ile ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho alikuwa Jaji Joseph Warioba mwaka 2014.

Mchakato huo uliishia kwa Rasimu Inayopendekezwa mwaka 2014. Tangu wakati huo kumekuwa na mjadala wa wapi ianzie, wapo wanataka iendelee kwa kura ya maoni na wengine wakitaka irejee kwa rasimu ya Jaji Warioba.

Pia, kuna wanaotaka iundwe timu itakayochakata rasimu na Katiba Inayopendekewa, ili kufanya maboresho na kupata sehemu nzuri ya kuanzia.

Akijibu swali kuhusu Katiba mpya, Kaunda amesema: “Tayari kuna rasimu ya Katiba na kwamba nitakapokuwa rais nitaishauri Serikali kuendelea na mchakato wa ile ya Jaji Warioba.”

Kuhusu matukio ya utekaji, Kaunda amesema ataishauri na kuisisitiza Serikali iunde tume ya kijaji kushughulikia masuala hayo.

Alijibu hilo huku akitolea mfano wa tume iliyoundwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere baada ya mauaji ya wazee na kusababisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi ajiuzulu.

“Nitakapokuwa rais nitahakikisha nashinikiza na kuishauri Serikali kuunda tume ya kijaji, ije ifanye uchunguzi kujua nini sababu,” ameeleza Kaunda.

Kwa upande wake, wakili Nkuba kuhusu Katiba ni kile alichoeleza kuna upungufu na kwamba atashauri kufanywa marekebisho.

Katika hoja hiyo, Nkuba amesema kwa wakati uliopo, kunahitajika kufanywa marekebisho ya Katiba kwa kuwa iliyopo ilifungwa kuendana na mahitaji ya zamani.

Wakili Nkuba amesema ataishauri Serikali kukwamua mchakato wa Katiba uliokwama mwaka 2014, ili uendelee.

Kwa upande wa matukio ya utekaji, amesema anakerwa na atakapopewa ridhaa ya kuwaongoza mawakili ataishauri Serikali kuunda sheria kali dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo.

Kuhusu ulinzi wa rasilimali za Taifa, ameeleza atakapokuwa rais ataishauri Serikali kutumia vizuri mawakili waliopo katika majadiliano ya masuala ya mikataba ya kimataifa, ili kuleta tija.

“Tatizo la Taifa kukosa faida katika mikataba linasababishwa na mikataba hiyo inaingiwa kibiashara na Tanzania haina nguvu ya kujadiliana vema, ili ipate faida,” amesema.

‘Rais wa TLS hana mamlaka’

Kuhusu Katiba mpya, wakili Muga amesema haoni kama rais wa TLS ana mamlaka ya kufanikisha upatikanaji wake, hivyo kuahidi hilo ni kuwaongopea wapiga kura.

Vivyo hivyo, ameeleza hata katika matukio ya utekaji, akisema aghalabu hufanyika gizani na rais wa TLS hana mamlaka ya kudhibiti isipokuwa atajadiliana na wanachama kuona namna ya kutatua.

Kuhusu rasilimali za nchi, Muga aliyejifananisha na Rais wa awamu ya tatu, Ali Hassan Mwinyi maarufu Mzee Rukhsa akisema kunahitajika juhudi za pamoja kuanzia kwa wananchi, kisha mawakili watasimama nyumba yao kufanikisha ulinzi wake.

“Kwenye ulinzi wa rasilimali si jambo la mtu mmoja, mwananchi naye ana nafasi yake, wananchi wakisimama nasi mawakili tukawa nyuma yao tutafanikiwa,” amesema Muga.

Kuuli naye msimamo wake ni kupatikana kwa Katiba mpya, akiahidi kusimamia kifungu cha nne cha sheria ya mawakili, kitakachompa jukumu la kuishauri Serikali.

Kuhusu masuala ya utekaji, ameeleza tatizo lipo kwa vyombo vya dola vinayojikuta vikisubiri matukio yatokee ndiyo viyakabili badala ya kuyadhibiti kabla.

Kuuli  amesema atakapokuwa rais wa TLS, ataishauri Serikali juu ya mwenendo mzuri wa kuyakabili matukio hayo.

Kama atakavyoshauri kuhusu matukio ya utekaji, amesema ataishauri pia katika ulinzi wa rasilimali za Taifa.

Suala la upatikanaji wa Katiba mpya kwa wakili Mwabukusi, amesema haitakuwa mzaha, ataliomba kwa njia zote ikiwamo kuwatumia wananchi kusukuma upatikanaji wake.

Mwabukusi amesema hatatumia njia moja kufanikisha mambo yenye masilahi ya Taifa, yapo atakayoshauri na mengine kwenda mahakamani na hata kuwaleta wananchi.

“Kuna jambo la kushauri na kuna vingine tutawaambia Watanzania, tuingie kutafuta haki hatutatumia njia moja kupata haki,” amesema Mwabukusi aliyerejeshwa kwenye mbio hizo za urais na Mahakama, baada ya kuenguliwa na kamati ya rufaa ya uchaguzi.

Pia, ameeleza yatakayofanyika kukabili matukio ya utekaji, huku ulinzi wa rasilimali za Taifa, akiahidi kushughulikia kama ambavyo amekuwa akifanya hivyo kabla ya kuwa rais.

Kuhusu ulinzi wa rasilimali hizo, Mwabukusi ameeleza kuna sheria nzuri, lakini imekosa wasimamizi imara na atakachokifanya iwapo atapewa ridhaa ni kushinikiza utekelezwaji wake kwa mbinu mbalimbali.

Swali la kwanini wao ni bora kuwa rais wa TLS, ni liliulizwa kwa kila mgombea katika mdahalo huo na kwa upande wake, Bendera amejigamba kwa uzoefu wa miaka 18 ya kutekeleza shughuli za uwakili.

Bendera amesema ubora wake haujengwi na uzoefu wa kutumikia uwakili pekee, bali unajengwa pia na wasifu wake wa kuongoza kampuni mbalimbali za uwakili.

“Najiamini kwa sababu ni mkongwe kwenye taaluma, uwakili na nimewahi kuziongoza kampuni za mawakili, nitatumia uzoefu wangu kuiongoza TLS,” ameeleza Bendera.

Jibu la uzoefu katika uongozi lilitolewa pia na Kaunda, akijinadi kuwa makamu wa rais wa mawakili Afrika na kuwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Uongozi wa TLS.

Hakuishia kuwa mzoefu tu, bali amesema ameshiriki kushauri mageuzi ya kitaasisi hasa kuleta utaratibu wa kuundwa kwa kanzidata ya mawakili na upigaji kura kwa njia ya kielektroniki.

“Kama nimeyafanya hayo nikiwa mjumbe wa baraza la uongozi, nikiwa rais nitafanya zaidi,” amesema Kaunda.

Ajivunia kuwa kiongozi toka shule ya msingi

Uzoefu wa uongozi pia, ulitajwa na Nkuba aliyesema amekuwa na nafasi hizo tangu akiwa shule ya msingi, sekondari na hata chuo kikuu, hivyo katika kuongeza hapaswi kutiliwa shaka.

Ubora wake, ameeleza unatokana na misimamo thabiti ambayo aghalabu huwa nayo na ndiyo inayofanya achaguliwe katika nafasi mbalimbali, hivyo anaomba akafanye hivyo na TLS.

Kuimarisha ushirikiano kati ya TLS na taasisi nyingine na kutengeneza fursa za mawakili wachanga, kadhalika kusimamia masilahi ya mawakili ni mambo mengine ikiwemo kwenda kuanzisha sera ya jinsia anayoitaja kama sehemu ya ubora unaomtofautisha na wengine.

‘Ajifananisha na Mzee wa Rukhsa’

Taaluma mseto alizonazo Muga, ndizo alizozitaja kama turufu bora kwake tofauti na wagombea wengine na kwa sababu hiyo anastahili kuwa rais wa TLS.

Mgombea huyo amesema mbali na taaluma ya uwakili, yeye pia ni mwanahabari aliyetumikia vyombo vya habari vya The Citizen, Daily News na BBC.

Taaluma hizo kwa mujibu wa Muga anayejifananisha na Mzee Rukhsa, zimemfanya kuwa na maarifa mseto, lakini amewahi kuwaongoza mawakili katika Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo suala la uzoefu nalo hapaswi kutiliwa shaka.

Kuuli yeye alilijibu swali hilo kwa kile alichoeleza, tofauti yake na wagombea wenzake ni uzoefu wa kimataifa aliokuwa nao, akisema anataka kuleta uzoefu wa kimataifa katika taaluma ya uwakili.

Amejinadi kwa wasifu wake wa kuwa wakili wa Mahakama mbalimbali za kimataifa, ikiwamo ya Haki za Binadamu na Afrika Mashariki.

“Nitakwenda kusimamia utawala wa sheria na heshima ya chama na hadhi na heshima ya wanachama, nina uzoefu wa kutosha,” amesema Kuuli.

Kwa upande wa Mwabukusi, uzoefu wa miaka 14 katika uwakili na miaka lukuki katika sekta ya sheria akaanza kuwa ofisa sheria ndani ya Serikali ni moja ya turufu zinazomtofautisha na wenzake.

Anajiona kustahili nafasi ya urais wa TLS kwa kile alichoeleza, amekuwa mdau wa haki za binadamu na utawala bora, kadhalika mtetezi wa wananchi katika maisha yake yote ya taaluma ya uwakili.

Ameshajihisha wasifu wake huo na harakati alizowahi kuzifanya, ikiwamo kupinga baadhi ya mambo yanayofanywa na Serikali kwa kuvunja haki za wananchi na masilahi ya Taifa.

“Naomba ridhaa nikayafanye haya nikiwa kiongozi wa mawakili. Nitasimamia vema na kuishauri Serikali kwa mbinu zote kuhakikisha masilahi ya Taifa na wananchi yanapatikana,” ameeleza Mwabukusi.

Katika mdahalo huo, Bendera aliulizwa iwapo kuna analojifunza kutokana na uamuzi wa Rais wa Marekani, Joe Biden kuamua kujiondoa katika harakati za kuwania urais kwa sababu ya umri wake.

Kwa mwonekano kati ya wagombea wote, Bendera ndiye anayeonekana kuwa na umri mkubwa zaidi na alijibu bado ana umri unaostahili kuwania nafasi hiyo.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts