Moshi. Waosha karoti katika eneo la Mto Karanga kwenye daraja la Bonite, Manispaa ya Moshi, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha eneo hilo, hatua ambayo itawawezesha kufanya kazi hiyo kwa ubora zaidi na katika mazingira salama.
Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti wakati wakiendelea na kazi hiyo ambayo ndiyo ajira yao, wamesema mazingira wanayofanyia kazi ni magumu kutokana na uwepo wa mashimo na matope katika eneo hilo, ambayo yamekuwa yakichangiwa na mvua zinazonyesha na kusababisha mto kujaa maji na kutapakaa pembezoni.
Idd Maganga, mmoja wa vijana wanaofanya kazi eneo hilo, amesema uboreshaji wa mazingira wanayofanyia kazi ni muhimu katika kuhakikisha wanaimarisha usalama wao wakati wote wawapo kazini.
“Mazingira tunayofanyia kazi siyo rafiki, kama kuna uwezekano wa kuboreshewa eneo hili tuboreshewe ili liwe bora zaidi wote tufanye kazi kwa usalama na uhuru.”
Ameitaja changamoto mojawapo inayowakabili ni magari kushindwa kufika eneo wanalooshea karoti na kupanga mizigo, hali ambayo inawafanya kubeba karoti kwa umbali mrefu kupeleka kwenye magari hivyo kupoteza muda mwingi kujaza gari moja.
Jeremiah Msumari amesema wanatamani eneo hilo liboreshwe kwa kuwekewa vifusi au zege, kwa kuwa wakati wa mvua wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatari.
Sabas Msofe, mmoja wa viongozi wa kikundi cha Juakali kinachosimamia shughuli za uoshaji karoti eneo hilo, amesema wanalipa fedha za matumizi ya maji ya Bonde la Pangani lakini hakuna mrejesho wa kuboreshewa mazingira ya eneo hilo.
“Changamoto kubwa kabisa ni kwamba tunalipa fedha Bonde la Mto Pangani kila mwaka, lakini haya mazingira tunaboresha wenyewe na mvua zikinyesha hali huwa mbaya zaidi kwa sababu ya mafuriko.”
“Tunaomba tuboreshewe eneo hili kwani kwa siku tunaosha karoti gari tatu au zaidi ambazo zinasafirishwa mikoa mbalimbali nchini tunapokea karoti kutoka Kilimanjaro na Kenya kulingana na msimu,” amesema Msofe.
Vick Lyimo, ambaye ni mnunuzi wa karoti katika eneo hilo, amesema gunia moja wanaoshewa kwa Sh3,000 licha ya mazingira kuwa ya ovyo.
“Tunafanyiwa bei hiyo kwa sababu waoshaji wanalalamikia mazingira mabovu, ina maana pakiboreshwa huenda bei ikashuka kidogo kwa kuwa hakutakuwa na usumbufu,” amesema Vick.
Mkurugenzi wa bonde afunguka
Akizungumza hilo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Segule Segule amesema hawatozi ada yoyote ya matumizi ya maji na kwamba watakaa na uongozi wa kikundi kinachosimamia eneo hilo kuona namna ya kuwashauri ili kuboresha mazingira yao ya kazi.
Akizungumzia usalama wa maji na chanzo hicho, Segule amesema uoshaji wa karoti ni jambo la kawaida kwa kuwa wanachoondoa ni udongo, ingawa tayari amemuelekeza mhandisi wa mazingira wa ofisi yake kuchukua sampuli ya maji ili kujiridhisha.