BAADA ya kuiwezesha Ceasiaa Queens kumaliza katika nafasi ya nne, kocha mkuu wa timu hiyo, Noah Kanyanga ameanza kuwindwa na Yanga Princess na huenda msimu ujao akakiongoza kikosi hicho cha Jangwani katika Ligi Kuu ya Wanawake nchini.
Kanyanga alikuwa na msimu bora huku akivuna alama nne kwa Yanga baada ya kushinda mchezo mmoja kwa bao 1-0 Da es Salaam kisha sare ya 2-2 walipokutana kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu.
Kama haitoshi kocha huyo ni miongoni mwa makocha watatu wanaowania tuzo ya kocha bora wa msimu wa 2023/24 ikiwa ni mara ya kwanza kwake kuingia katika orodha ya kinyang’anyiro hicho na kuweka rekodi na historia katika kazi yake.
Habari za ndani ilizopata Mwanaspoti ni kuwa tayari mabosi wa Yanga Princess wameshaanza harakati za kupata saini ya kocha huyo kumvuta Jangwani kwa ajili ya msimu ujao, ambapo mazungumzo ni kuvunja mkataba wa Kanyanga kwa Ceasiaa Queens.
Hata hivyo, alipoulizwa na gazeti hili kuwindwa na vigogo hao, kocha huyo alisema bado ni mapema huku akieleza mafanikio yake msimu uliopita akibainisha kwamba analo deni kubwa kwa timu yake msimu ujao.
Alisema baada ya kumaliza msimu, anahitaji kuanza maandalizi ya msimu ujao mapema ikiwa ni usajili na kambi ya maana kuhakikisha wanawania nafasi mbili za juu na kwamba kiu yake kubwa ni kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
“Haijawa rasmi, mimi ninao mkataba na Ceasiaa Queens na mipango yangu ni kuona napambania ubingwa msimu ujao, nitafanya usajili bora, kambi ya mapema na kupata mechi za kirafiki, kiujumla nashukuru ushirikiano ndani na nje ya uwanja,” alisema Kanyanga.
Alisema kuingia katika orodha ya makocha bora wa msimu, kwake ni mafanikio makubwa akieleza kuwa inaongeza ari na morali katika kazi yake ya soka kufikia ndoto zake, huku akiwapongeza nyota wake kwa kazi nzuri.