ACT Wazalendo kupinga mahakamani Tamisemi kusimamia uchaguzi

Musoma. Chama cha ACT Wazalendo kinatarajia kwenda mahakamani kupinga uchaguzi wa Serikali za mitaa kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Hii si mara ya kwanza kwa chama hicho kulalamikia uchaguzi huo kusimamiwa na Tamisemi, kwani Aprili 5, 2024 Waziri Mkuu kivuli wa chama hicho, Isihaka Mchinjita aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa hawatakubali kuona uchaguzi huo ukisimamiwa na Tamisemi, wakati kuna sheria mpya ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Julai 29, 2024 mjini Musoma, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema hitaji la vyama vya siasa, kikiwemo chama chake ni kuwa na Tume Huru ya Uchunguzi itakayosimamia kwa uhuru na haki uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.

Amesema wameshangazwa na hali ilivyo sasa, Serikali kupitia Tamisemi kuanza mchakato wa maandalizi ya kusimamia uchaguzi huo, jambo ambalo halikubaliki.

Amesema chama hicho kinatarajia kufikisha suala hilo mahakamni ndani ya wiki moja kuanzia sasa, ili Mahakama itoe zuio kwa Tamisemi kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi huo na badala yake usimamiwe na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

“Tumechelewa kwenda mahakamani kwa sababu tulikuwa tunasubiri kanuni za uchaguzi huo ambazo zimetangazwa wiki mbili zilizopita, hivyo kwa sasa wanasheria wetu kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wamejifungia wakifanya taratibu zote, hivyo ndani ya wiki moja nadhani tutakuwa tunalifikisha suala hili mahakamani,” amesema.

Katika hatua nyingine, Shaibu amesema chama hicho hakitaishia kuzungumzia changamoto za wananchi kwenye majukwaa ya kisiasa, badala yake watahakikisha changamoto hizo wanazifikisha kwa mamlaka husika, ili zifanyiwe kazi haraka.

Amesema mamlaka hizo ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na mamlaka nyingine, lengo ni kuona changanoto za wananchi zinafanyiwa kazi na kupata ufumbuzi kwa wakati.

Kwa kuanzia, amesema chama hicho kimewasilisha changamoto za wakazi wa Mkoa wa Mara kwa mkuu wa mkoa huo, Evans Mtambi  leo Julai 29, 2024 kutokana na ziara  waliyoifanya siku tano mkoani humo ambapo pamoja na mambo mengine wananchi waliwasilisha kero zao.

“Si kuzifikisha kero tu, bali kufuatilia hadi zifanyiwe kazi, kwani Watanzania wana changamoto nyingi na kusababisha wawe na maisha magumu bila sababu za msingi,” amesema.

Amesema katika ziara ya Mkoa wa Mara, wamebaini uwepo wa changamoto nyingi ambazo wamezifikisha kwa mkuu wa mkoa aliyeahidi kuzifanyia kazi ndani ya muda mfupi.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ubovu wa barabara, hasa maeneo ya vijijini, ukosefu wa maji safi na salama, licha ya mkoa kuwa na chanzo cha uhakika wa maji, viashiria vya ubadhirifu na rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maji, elimu na afya.

Changamoto nyingine ni usalama wa wavuvi ndani ya  Ziwa Victoria na wafugaji, utekelezaji wa sera ya matibabu bure kwa wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano, migogoro ya ardhi pamoja na fidia kwa watu ambao maeneo yao yamechukuliwa na Serikali kupisha utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Related Posts