Ajira za afya 9,483 kuelekezwa maeneo ya pembezoni

Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kutokana na uhaba uliopo wa watumishi wa afya maeneo ya pembezoni mwa nchi, ajira mpya 9,483 zilizotangazwa zitaelekezwa maeneo hayo.

Amesema watumishi hao watapelekwa katika halmashauri za pembezoni mwa nchi ili kupunguza uhaba wa wataalamu hao unaokadiriwa kuwa ni zaidi ya asilimia 50.

Upungufu huo unaozikabili zahanati na vituo vya afya na baadhi ya hospitali za halmashauri, umechangia kudhoofisha hali ya utoaji wa huduma za afya nchini.

Amesema ili kuweka mazingira mazuri ya kazi, tayari Serikali imeanza kutafuta mwarobaini kuhakikisha watumishi wanaoajiriwa maeneo hayo wanakwenda na wanabaki huko kwa kupelekewa huduma muhimu ikiwamo shule, umeme, maji na nyinginezo.

Waziri Ummy amesema hayo leo Jumatatu Julai 29, 2024 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi la Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Mkapa linalofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

“Kuna changamoto tunaajiri sana lakini tatizo bado liko palepale kwa sababu tumejenga sana zahanati, huduma za kibingwa, vituo vya afya na changamoto kubwa ipo katika ngazi ya chini zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri.

“Kila mwaka sekta ya afya tunapata vibali vya kuajiri watumishi, hivi sasa tumetangaza ajira mpya. Uhaba upo katika maeneo ya pembezoni, bahati mbaya tunaowaajiri wengi wanataka wabaki Dar, Dodoma, Arusha na maeneo mengine ya mijini hii changamoto tunayopambana nayo,” amesema Waziri Ummy.

“Na nimeongea na waziri mwenzangu Mohamed Mchengerwa (wa Tamisemi) kwamba tutasema wewe unapaswa kwenda Halmashauri ya Uvinza ambako ndiko kuna uhaba zaidi wa watumishi, kwahiyo tunatoa wito kwa watumishi wa afya kwenda huko zaidi.”

“Niwatoe hofu watumishi wa afya kutoogopa kufanya kazi katika maeneo ya pembezoni mwa nchi kwa kuwa huduma zote muhimu za kijamii zinapatikana ikiwamo umeme, barabara, maji pamoja na shule ambazo Tamisemi sasa wanajenga za mchepuo wa Kiingereza kwa ajili ya wale wanaotaka watoto wao wasome huko,” amesema Waziri Ummy.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za afya Tanzania (Aphtha), Dk Samwel Ogillo amesema kwa sasa kuna madaktari zaidi ya 5,000 wapo mtaani hawana kazi, nafasi za ajira wanapoomba wengi hawapati kazi na wengine wanajitolea bure.

“Wakiajiriwa wataenda, tatizo wakiingia mfumo wa ajira anaanza kufanya mpango wa kuhama, ila watengenezewe mazingira mazuri ili wakienda huko wasiondoke, vijana wengi ni wadogo wataishi huko bila shida, wapo tayari waboreshewe mazingira tu,” amesema.

Mkunga kutoka Chama cha Wakunga Tanzania (Tama), Lucy Madaba amesema mkunga mmoja anatakiwa ahudumie wajawazito wanane, lakini uhalisia maeneo ya pembezoni anahudumia 15 mpaka 20 akiwa peke yake.

“Tunapenda Serikali iangalie upande wa kuajiri wakunga kwa sababu malengo yetu ni kupunguza vifo vya mama na mtoto, lakini changamoto kubwa maeneo yetu hasa vijijini unaweza kufika kwenye vituo unakuta mkunga yuko mmoja ana anahudumia mjamzito mpaka anapojigungua, hili lifanyike ili ufanisi wa kazi uende inavyohitajika,” amesema Madaba.

Akizungumzia kongamano hilo, Waziri Ummy amesema mkutano wa leo unajadili masuala ya rasilimali watu kwenye sekta ya afya ambao ni uzalishaji wa wataalamu wa afya ndani ya nchi, ubora wa watumishi  kwa kuhakikisha watumishi wanasalia kwenye maeneo waliyopangiwa kuhudumia wananchi.

Waziri Ummy amesema hayati Mkapa alikuwa kinara waliofanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya ikiwamo Sheria ya Bima ya Afya ya NHIF aliyoiasisi Mwaka 2000.

Amesema, hivi sasa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa ndio chanzo kikuu cha mapato yanayotokana na huduma zinazotolewa kupitia mfuko huo.

Kongamano hilo linalokutanisha wadau mbalimbali katika sekta ya afya ambao watajadili masuala mbalimbali, linatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho Jumanne Julai 30, 2024 na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa. Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020, Dar es Salaam na kuzikwa Lupaso, wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara.

“Tunategemea kupata maoni na ushauri wa wadau mbalimbali wa afya ikiwamo sekta binafsi katika kutengeneza mkakati wa sita wa Taifa wa Sekta ya Afya Mwaka 2026/2031 ambao inaendana na kukamilisha kwa Dira ya Taifa ya Mwaka 2050,” amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mkapa, Dk Hellen Mkondya amesema rasilimali watu ni muhimu sana hasa katika wakati huu ambao nchi inaelekea katika bima ya afya kwa wote.

Akizungumza wakati wa mdahalo wa mabalozi kuhusu mada hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Makocha Tembele amesema katika mafanikio ambayo Indonesia wanayo kwenye sekta ya afya ni kwenye suala la bima ya afya.

Amesema pamoja na kwamba wana watu milioni 270 lakini wamefanikiwa kutoa bima ya afya kwa watu milioni 210 sawa na asilimia 81 ya nchi hiyo tangu walipoanza mwaka 2014.

“Wamekwenda haraka sana na ni eneo ambalo tunajifunza. Walichokifanya wameunganisha mfumo wa afya na mtandao, kwahiyo kuna huduma hauhitaji kwenda hospitali kama unajisikia una mafua unampigia simu daktari anakuunganisha kwenye mfumo mnaongea kwa zoom anakupatia dawa na unapelekewa hadi nyumbani unalipia gharama za usafiri. Inapunguza presha ya kwenda kwenye vituo vya afya,” amesema Tembele.

Related Posts