Arusha. Mahakama Kuu ya Mtwara imemhukumu kifungo cha miaka mitatu na miezi sita jela, Hadija Issa (55), mkazi wa mkoani Lindi, baada ya kumkuta na hatia ya kuua bila kukusudia.
Hadija alidaiwa Julai 17, 2023, mkoani Lindi, akiwa analinda ufuta shambani kwake, alisikia mtu anakohoa na alipofuatilia sauti alimuona akichimba viazi vitamu shambani kwake na kuvitia kwenye mifuko.
Ilidaiwa ghafla Simon Ngurumo (marehemu) alimvamia mshtakiwa na kumpokonya panga na kumrushia, mshtakiwa alilikwepa lakini lilimjeruhi kidole gumba.
Wakati wakiendelea kupigana, ilidaiwa mshtakiwa alifanikiwa kumnyang’anya Ngurumo panga lake na kumshambulia kwa kumkata kichwani, mkononi na miguuni, hali iliyosababisha atokwe damu nyingi na kufariki dunia.
Uamuzi huo umetolewa Julai 24, 2024 na Jaji Martha Mpaze, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, aliyeeleza kuwa baada ya mshtakiwa kukiri kosa, Mahakama inampunguzia adhabu kwa kumhukumu kifungo cha miaka mitatu na miezi sita jela.
Awali, Hadija alipandishwa mahakamani hapo Machi 27, 2024 na kusomewa shtaka la mauaji, alikiri kosa.
Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, siku ya tukio saa nne asubuhi, mshtakiwa alikwenda kuripoti kwa Mwenyekiti wa Mtaa, Ashura Ngambe ambaye aliongozana naye na watu wengine na walipofika shambani, walimkuta Ngurumo amepoteza fahamu.
Tukio hilo liliripotiwa Kituo cha Polisi Lindi na maofisa wa polisi waliongozana na daktari na walipofika eneo la tukio, alibaini Ngurumo amefariki dunia kutokana na kupoteza damu nyingi.
Ilidaiwa mshtakiwa huyo alipokamatwa, alikiri kumkata kwa panga kichwani na sehemu nyingine za mwili na kwamba tukio hilo lilitokea wakati wa mapigano kwa sababu marehemu alikwenda kuiba shambani kwake.
Upande wa mashtaka ulitoa ripoti ya uchunguzi wa mwili, cheti cha kukamata na maelezo ya mshtakiwa ya kukiri, hivyo Mahakama kumtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Wakili aliyemwakilisha Hadija, aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu mteja wake kwa sababu hana rekodi ya uhalifu na hilo ni kosa lake la kwanza.
Alieleza kuwa pia ameonyesha ushirikiano tangu alipokamatwa, hakukimbia baada ya tukio na ameonyesha kujutia kosa lake. Pia ana watu wanaomtegemea.
Wakili huyo aliiomba Mahakama kuzingatia namna kosa hilo lilivyotendwa, akionyesha haikuwa nia ya mshtakiwa kulitenda, ila alijikuta ametenda kwa kujilinda na kuomba Mahakama impunguzie adhabu ikiwezekana iwe adhabu ya nje, ili aitunze familia yake.
Kwa upande wake, wakili wa upande wa mashtaka aliomba Mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria, ili iwe fundisho kwa wengine akidai mshtakiwa amesababisha kifo cha kijana anayetegemewa na familia yake.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Martha alieleza kwa mujibu wa kifungu cha 198 cha Kanuni ya Adhabu, adhabu ya kosa la mauaji ni kifungo cha maisha jela na kuwa kifungu hicho hakitoi adhabu ya chini.
Amesema kwa kuangalia mazingira ya kosa na namna lilivyotendeka anaona liko chini ya kiwango cha juu, ila kwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa kwa kutumia silaha, hatua yake ni kuanzia miaka 14 jela.
Jaji alieleza kwa kuzingatia punguzo la adhabu kuwa mshtakiwa alikuwa akijitetea na mali zake, mwongozo unaonyesha ikiwa mtu atatumia nguvu kupita kiasi katika kudai haki au kujilinda au mali, huangukia adhabu ya chini hadi miaka minne.
“Kwa hivyo, nitapunguza kifungo kwa miaka minne na kuacha miaka 10 kwa kuzingatia kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza, ana familia inayomtegemea, ana umri wa miaka 55, ninapunguza kifungo kwa miaka miwili na kuacha miaka minane.
“Zaidi ninaendelea kupunguza mwaka mmoja kwa ushirikiano wake tangu wakati wa tukio, kukiri kwake na hajakimbia eneo la tukio, hukumu sasa ni miaka saba,” alifafanua.
Jaji Martha alieleza iwapo mshtakiwa asingekubali hatia, angemhukumu kifungo cha miaka saba jela, hivyo anapunguza theluthi moja ya adhabu na kuifanya iwe miaka minne na miezi saba na akasema anapunguza pia miezi 13 aliyokaa kizuizini.
“Kwa hivyo, uamuzi wangu wa mwisho wa hukumu, ninamhukumu Hadija kutumikia kifungo cha miaka mitatu na miezi sita jela,” alihitimisha Jaji Martha.