KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars (SBS), Patrick Aussems amesema bado anaendelea kusuka kikosi cha ushindani kwa kutumia mechi za kirafiki huku akidai timu hiyo ipo tayari, lakini kazi ni kwake kusaka kikosi cha kwanza.
Aussems amefunguka hayo siku chache baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dodoma jiji ambapo amedai kuwa ameanza kusuka safu ya ushambuliaji kabla ya kumalizana na mabeki.
“Tumepata wakati mzuri wa kushiriki Kagame Cup. Licha ya timu kutokuwa na nafasi nzuri ya maandalizi mashindano hayo yametuonyesha ni sehemu gani tuna upungufu,” alisema kocha huyo na kuongeza:
“Juzi tumecheza na Dodoma Jiji sikuwa nazingatia zaidi matokeo, nilipanga kikosi nikiangalia zaidi mfumo gani nitaweza kuutumia baada ya ligi kuanza. Kwenye mchezo huo nilianza na washambuliaji wawili lengo ni kuwajenga.”
Alisema amebaini safu ya ushambuliaji ipo vizuri katika kutengeneza nafasi, lakini shida ni umaliziaji hivyo mchezo ujao dhidi ya Namungo FC, Agosti Mosi, atatumia mshambuliaji mmoja na kutumia mfumo wa kujilinda ili kubaini upungufu wa ukuta wake.
“Nitafanya hivyo kwa lengo la kuona ukuta wangu una shida sehemu gani na natakiwa kuboresha nini kabla ya ligi haijaanza ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuonyesha ushindani kwa wapinzani,” alisema.
Kocha huyo ambaye aliwahi kuinoa Simba na amejiunga na Singida Black Stars katika dirisha hili, alisema kwa ujumla kikosi chake kipo kwenye nafasi nzuri ya ushindani na kilichobaki ni kupambana kusaka kikosi cha kwanza.
“Kwa asilimia kubwa wachezaji wameweza kuonyesha ni namna gani wanahitaji namba kikosi cha kwanza na wapo kwenye utimamu mzuri wa kimwili. Kazi inabaki kwangu mimi nani anatakiwa kuanza na nani anatakiwa kucheza kikosi cha pili,” alisema.
Singida Black Stars mbali na mechi za Kombe la Kagame hadi sasa imecheza mechi tatu za kirafiki ikianza na Polisi Tanzania ikashinda 3-0, dhidi ya ACA Eagles sare ya mabao 2-2 na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dodoma Jiji.