Dk Nchimbi: Serikali ifanikishe upatikanaji wa masoko, pembejeo kwa wakulima

Mtwara. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ameielekeza Serikali kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati, kwa bei nafuu pamoja na masoko ya mazao ya wakulima yanapatikana.

Dk Nchimbi ametoa wito huo leo Jumatatu Julai 29, 2024 wakati akisalimia wananchi wa Kata ya Mpapura, Mtwara Vijijini akiwa njiani kuelekea mkoani Lindi.

Ameipongeza Serikali kwa jitihada inayofanya kuhakikisha wananchi wanapata pembejeo za kilimo, ili kuongeza uzalishaji wao. Hata hivyo, amesisitiza pembejeo hizo zitolewe kwa wakati na kwa bei nafuu.

“Serikali ihakikishe pembejeo zinapatikana kwa wakati, kwa bei nafuu na pia ihakikishe masoko ya mazao ya wakulima yanapatikana,” amesema Dk Nchimbi.

Kuhusu Bandari ya Mtwara, katibu mkuu huyo ameeleza kufurahishwa na uboreshaji uliofanyika kwa uwekezaji wa Sh150 bilioni, jambo litakaloongeza mapato ya banda ri hiyo kwa zaidi ya Sh23 bilioni.

“Serikali iendelee kufanya uwekezaji kwenye bandari hii, ili kupunguza mzigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Tumeona ufanisi wa bandari hii ulivyopunguza mzigo,” amesema Dk Nchimbi.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameishukuru Serikali kwa kuanzisha kongani ya viwanda vya korosho ambapo Sh73 milioni zimetengwa kwa ajili ya mradi huo na tayari mkandarasi yupo eneo la mradi.

“Tunaishukuru Serikali kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa kwenye wilaya yetu. Tuna mradi wa ukarabati wa vituo vya afya, ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri na miradi ya maji, kazi kubwa inafanywa na Serikali yetu,” amesema.

Mmoja wa wakazi wa Kata ya Mpapura, Said Ngwali amesema wanakabiliwa na migogoro ya ardhi, hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia wapate maeneo ya kulima, ili kuendesha maisha yao.

“Tunaomba Serikali itusaidie kuondokana na migogoro hii, tunashindwa kufanya mambo ya maendeleo, hivyo tunabaki maskini,” amesema mwananchi huyo.

Akizungumzia migogoro ya ardhi katika kata hiyo, Dk Nchimbi amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Patrick Sawala kushughulikia jambo hilo.

Related Posts