HISIA ZANGU: Gamondi bado ni jeuri, Kaizer wameonyeshwa walipo

HATUJUI sana mbele ya safari, lakini wote tuliona namna ambavyo Kaizer Chiefs waliteketea mbele ya Yanga katika dimba la Bloemfontein pale Afrika Kusini. Kilikuwa kichapo kikali mbele ya mashabiki wao. Mabao 0-4. Kuna mambo ambayo tunaweza kuchukua peni na kuandika.

Kwanza Kaizer Chiefs wamewekwa katika nafasi yao na Yanga. Kwamba kwa sasa Yanga wapo katika hadhi ya kina Mamelodi Sundowns na sio tena Kaizer Chiefs na Orlando Pirates. Hawa Mamelodi wamewekeza pesa nyingi kiasi cha kuziacha nyuma Orlando Pirates na Kaizer Chiefs. Yanga na Simba sasa hivi wanatamani kuwa kule juu.

Dalili kwa Yanga zilianza kujionyesha wakati bao la Aziz Ki lilipokataliwa pale Pretoria. Yanga walikuwa wanaitoa Mamelodi katika pambano lile na wangeweza kusonga mbele. Hapo Yanga walikuwa wanajiweka katika hadhi ya Mamelodi. Kama unaweza kupambana na Mamelodi kwanini usiiadhibu Kaizer Chiefs ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya 10 katika Ligi Kuu Afrika Kusini.

Labda wanaweza kurudi tena siku za usoni, lakini kwa sasa Kaizer wapo chini ya Yanga. Sijawatazama vyema watani zao Orlando Pirates, lakini kwa nilichokiona juzi, Nasreddine Nabi na mabosi wa Kaizer wanapaswa kufahamu kwamba kuna timu kutoka Afrika Mashariki ipo juu yao kwa sasa. Hata mashabiki wa Kaizer wameshuhudia hivyo.

Lakini ndani ya uwanja kocha Miguel Gamondi wa Yanga ameendelea kuonyesha jeuri na akili ambayo nilitazamia kocha yeyote mwenye akili timamu aionyeshe. Gamondi amejaziwa mastaa wengi katika kikosi na bahati nzuri hatumii akili za mashabiki kufanya mambo yake.

Katika hizi mechi amefanya mambo mawili makubwa. Kwanza kabisa ni kubadilisha wachezaji kwa sababu mbalimbali. Kwa mfano, pambano dhidi ya Ausburg Khalid Aucho na Kennedy Musonda hawakucheza. Kisa? Walichelewa kuanza mazoezi na wenzao. Nadhani walikuwa na ruhusa maalumu, lakini haiondoi ukweli kwamba walikuwa nyuma katika ratiba ya mazoezi.

Ikanifurahisha pia katika pambano la pili dhidi ya TS Galaxy. Sijui ilitumika akili yake binafsi kuwapanga wachezaji wazawa tupu katika kipindi cha kwanza. Hakuna kitu cha maana ambacho tulikiona. Inanikumbusha kelele ambazo tumekuwa tukipiga. Eti kwamba tupunguze idadi ya wachezaji wa kigeni. Ukweli ni kwamba tukicheza wenyewe bado kuna mambo mengi tunakosa.

Gamondi alikuwa anatupa ujeuri wake katika kile ambacho tumekuwa tunafikiria. Simba ingeweza kufika robo fainali nne mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutumia wazawa tupu? Isingewezekana. Yanga wangeweza kufika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika kwa kutumia wazawa watupu? Isingewezekana. Huu ni ukweli mchungu.

Walipoingia kina Prince Dube katika kipindi cha pili ndio wakaweza kurekebisha mambo kwa haraka. Dube akafunga bao la mapema kipindi cha pili, Yanga wakashinda mechi yao ya mpira wa miguu. Huu ndio ukweli ambao lazima tuumeze. Dube alipata nafasi moja tu akarebisha mambo.

Mechi ya Kaizer Chiefs Gamondi alitupa ujeuri wa namna mbili. Kwanza kilikuwa ni kikosi ambacho kiliendelea kubadilika kutokana na mahitaji uwanjani. Ile ndoto ya mashabiki kuwaona Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Azizi Ki wakicheza kwa pamoja imezidi kutokomea. Gamondi anatumia akili yake na sio ya  mashabiki.

Timu inahitaji uwiano wa kushambulia na kujihami.  Inahitaji wachezaji ambao watatia nguvu katika ukabaji. Katika roho hii kuna Duke Abuya, Aucho, Clement Mzize. Dube na Aziz Ki wanaweza wasiwe wakabaji sana, lakini nyuma yao kuna watu wanaoweza kukimbiza zaidi mipira. Timu ya mpira wa miguu inatakiwa hivi.

Na hata katika kuleta uwiano unahitaji atoke Aziz Ki aingie Chama. Atoke Duke Abuya au Aucho ili aingie kiungo mwingine mkabaji kama Mudathir Yahya au Aziz Andambwile. Hivi ndivyo mpira wa kisasa ulivyo. Mambo ya kupanga galacticos kwa pamoja kwa ajili ya kufurahisha mashabiki yamepitwa na wakati. Yaliwahi hata kuwagharimu Real Madrid.

Lakini hapohapo Gamondi ameendelea kuwa jeuri kwa namna ambavyo anataka wachezaji wake watimize majukumu  wasipokuwa na mpira. Huu umeendelea kuwa ubora wa Yanga kwa muda mrefu. Kuanzia wakati wa Nabi hadi wakati huu wa Gamondi. Bahati nzuri kwa Yanga ni kwamba Gamondi anaonekana kuwa master zaidi. Kaizer wangeweza kucheza siku mbili wasione nyavu za Djigui Diarra.

Kila mmoja alikaba. Kuanzia juu, katikati hadi chini. Hii huwa inaanzia mazoezini. Unahitaji kocha wa viungo ambaye anawafua zaidi wachezaji ili waweze kuwa bora wakati hauna mpira. Ndivyo ambavyo imewafanya Manchester City, Liverpool na Arsenal kuwa bora zaidi katika miaka ya karibuni. Kuonyesha ubora wako wakati hauna mpira.

Kazi ya kuwanyoosha inakuwa ngumu zaidi pale unapokusanya wachezaji mastaa. Mara nyingi kama una kundi kubwa la mastaa huwa wanafurahi zaidi kuuchezea mpira kuliko kukaba. Kazi ya kocha wa kisasa ni kuwanyoosha na kuwataka wakabe sawa katika kiwango kilekile ambacho wanakitumia wakiwa na mpira. Sio kazi nyepesi. Mastaa hawapendi sana.

Juzi Kaizer Chiefs sio tu kwamba walikuwa wanapata tabu wakati Yanga walipokuwa na mpira, lakini pia walikuwa wanapata tabu wakiwa na mpira. Yanga walikuwa wanafanya ‘pressing’ ya hatari. Nadhani Chama itabidi aingie katika mfumo wa kocha. Sioni sana kama Yanga wataingia katika mfumo wake.

Na sasa tumeshaiona Yanga kwa mechi tatu. Wanarudi na taji lao la Toyota baada ya kuwasha moto pale Bloemfontein. Inatia hamu kusubiri kuona watani wao wamejiandaaje. Kuanzia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kwa wale ambao ndio kwanza wameingia kikosini hadi uwezo binafsi wa kocha na mipango yake.

Wiki hii tutapata mwanga katika mechi za ufunguzi wa msimu ndani ya klabu. Simba Day na Wiki ya Mwananchi. Halafu baada ya hapo watakutana wenyewe kwa wenyewe siku ya Nane Nane. Haitajalisha sana kuhusu matokeo, kitu ambacho tutataka kujua ni nani amefikia wapi kiuwezo.

Yanga wameonekana kuimarika zaidi, lakini hata kama Simba watakuwa hawajawafikia Yanga tunataka kujua na wao wamesogea kutoka wapi hadi wapi. Hata mashabiki wao wamekuwa na kiu kubwa ya kujua kuhusu jambo hilo. Siku chache zijazo zitakuwa hakimu mzuri zaidi.

Related Posts