Mwanza. Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Athman Matuma amewajia juu mawakili wawili na kulaani kitendo chao cha kughushi nyaraka zilizowasilishwa mahakamani kumuombea dhamana mshtakiwa wa kesi ya mauaji bila kukusudia.
Hata hivyo, ili kulinda majina yao, jaji hakuwataja majina yao halisi mawakili hao, isipokuwa aliwapa majina ya uongo ya ‘Chapu Chapu’ na ‘Kazi ni Kazi’, akisema walichokifanya si tu ni ukiukaji wa madili ya uwakili, bali ni kosa la jinai.
Jaji Matuma ametoa msimamo huo leo Jumatatu Julai 29, 2024 Jijini Mwanza, wakati akitoa uamuzi mdogo kuhusiana na maombi ya dhamana ya mshtakiwa Gerevas Kalikanywe, anayekabiliwa na shtaka la kumuua bila kukusudia, Pascal Seni.
Mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya kesi hiyo ambayo alidaiwa Aprili 19, 2023 eneo la Nyamanoro, alisababisha kifo cha Pascal, kosa ambalo lina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hivyo, wakili wake akawasilisha maombi Mahakama Kuu kwa ajili ya dhamana, lakini kila shauri hilo lilipoitwa kortini, ni wakili wake tu ndiye aliyekuwa akihudhuria na kusisitiza maombi hayo yasikilizwe bila mshtakiwa huyo kuwapo.
Katika uamuzi wake huo, Jaji amesema ameshuku juu ya shinikizo lisilo la kawaida kwa kuwa mara zote kesi ikiitwa, wakili huyo amekuwa akiambatana na watu mbalimbali waliotambulishwa mahakamani kama ndugu wa mshtakiwa huyo.
Jaji alivyowabana mawakili
Hata hivyo, pamoja na shinikizo kutoka kwa mawakili hao, Jaji alisisitiza lazima mshtakiwa afike mwenyewe kortini, ili kuithibitishia Mahakama kama kweli ameomba dhamana kupitia maombi hayo na kama wanaokwenda kortini ni ndugu zake.
Kutokana na mashaka kuongezeka, Jaji Matuma aliamua kufuatilia kwa umakini mwenendo wa shauri hilo na kushuku kuwa kiapo kilichodaiwa kuapwa na mshtakiwa, kilitiwa saini na mtu aliyejitambulisha ndiye aliyekiandika.
“Hii maana yake ni wakili ndiye alisaini akijifanya ndiye mleta maombi. Kutokana na hilo nilimwamuru wakili aieleze Mahakama kama ni kweli mshtakiwa ndiye alisaini hati hiyo ya kiapo,” alieleza Jaji Matuma katika uamuzi wake huo.
Akinukuu majibu yake, Jaji alisema aliieleza Mahakama kuwa baada ya kuandaa nyaraka, aliwapa ndugu wa mshtakiwa kuzipeleka gerezani, ili mshtakiwa azisaini, walizichukua na baadaye kuzirudisha zikiwa zimesainiwa naye kuzipeleka kortini.
Baadaye alimweleza Jaji kuwa ndugu aliyempa nyaraka hizo yupo mahakamani na anaitwa Ruben Gaudence, ingawa ndugu huyo alipotakiwa kutoa maelezo yake, alisema hakushuhudia mshtakiwa akisaini nyaraka hizo.
Akimnukuu ndugu huyo, Jaji alisema wala hakuwahi kupokea hizi nyaraka kutoka kwa wakili na kwamba ni Nashon Kalikwenye aliyezichukua na wala hakumsindikiza ndugu huyo gerezani kwa ajili ya kumsainisha Gerevas Kalikwenye.
Mshtakiwa aitwa, mazito yaibuka
Baada ya kusikiliza maelezo kutoka kwa wawili hao, Jaji Matuma aliagiza mshtakiwa aletwe kutoka gerezani, ili kuthibitisha kama saini iliyopo katika kiapo hicho ni yake.
Wakili aliyepewa jina la ‘Kazi ni Kazi’ ndiye aliyedai kushuhudia kiapo wakati wakili aliyepewa jina la ‘Chapu Chapu’ ndiye aliyeandaa nyaraka hizo.
Shauri hilo lilipokuja kusikilizwa kutokana na amri hiyo ya Jaji, mawakili hao wawili walifika mbele ya Jaji Matuma, huku mshtakiwa aliwakilishwa na wakili wa Serikali, Christopher Olembile ambapo hapo ndipo mambo yalipojulikana wazi.
Wakili ‘Chapu Chapu’ alifunguka kuwa ni kweli mshtakiwa si aliyesaini nyaraka hizo na kwamba yeye na wakili mwenzake wanaiomba radhi Mahakama kwa makosa waliyoyatenda na kwa msingi huo, maombi hayo yalikuwa batili.
“Sisi bado ni mawakili wachanga na tunaendelea kujifunza. Tunajuta kwa tulilolifanya na tunaomba msamaha. Kusema ukweli mimi ndiye nilisaini hati ya kiapo kwa nia njema, ili kuharakisha muombaji apate dhamana,”alieleza wakili huyo.
Kwa upande wake, Wakili ‘Kazi ni Kazi’ naye aliomba msamaha kwa kile alichokifanya na kwamba kama wakili alipaswa kuwa makini na kueleza nyaraka hizo zililetwa ofisini kwake na wakili mwenzake ‘Chapu Chapu’.
Jaji akanukuu alichokisema; “Pamoja na hayo naomba kusema mimi bado ni wakili mchanga ambaye nina muda mwingi wa kuendelea kujifunza. Nitahakikisha najirekebisha na kutenda kwa ubora zaidi. Naomba msamaha.”
Ndugu walivyowachoma mawakili
Ruben Gaudence na Nashon Kalikwenye, waliiambia Mahakama kuwa wao walichokifanya ni kufika kwa wakili na kumkodi kushughulikia dhamana ya ndugu yao na aliwaambia angeshughulikia suala hilo.
Ndugu hao wakaeleza kuwa walisubiri hadi walipojulishwa na wakili kwamba tayari maombi yamefunguliwa kortini na kujiweka kando na kugushi saini ya mshtakiwa na kwamba wakili hakuwaambia lolote kuhusiana na kuweka saini.
Muombaji ambaye ndiye mshtakiwa, alikana kughushi nyaraka hizo, lakini akawaombea msamaha mawakili hao akisema anaamini walifanya makosa hayo kwa nia njema na kusisitiza hajawahi kusaini nyaraka hizo za kiapo.
Wakili wa Serikali kwa upande wake baada ya kusikiliza hoja hizo, alijenga hoja kuwa maombi hayo kwa mazingira hayo ni batili mbele ya macho ya sheria, lakini akasema kwa suala la ukiuakaji maadili wa mawakili anaiachia Mahakama.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji alisema analaani tabia ya baadhi ya mawakili na wateja wao kutokuwa waaminifu kwa Mahakama na kuiingiza katika mashauri yanayoegemea nyaraka zilizoghushiwa.
Alisema nia njema si utetezi katika ukiukwaji wa maadili kwa kuwa zipo njia za kisheria ambazo zinaweza kufuatwa bila kukiuka maadili ya uwakili.
“Imegeuka ni tabia sasa kwa mawakili kutumia njia ya mkato ambayo ni haramu kisheria. Kwa kufanya hivyo unaitumbukiza Mahakama kushughulikia nyaraka ambazo ni za kughushi ambazo zinanyima haki,” alieleza Jaji Matuma.
“Nimesikiliza maombolezo ya mawakili waliyoyawasilisha mbele yangu kwamba bado ni vijana katika fani, hivyo wasamehewe kwa ukiukwaji huo wa maadili, ili waendelee kujifunza zaidi, lakini nimeamua kuandika uamuzi huu.
“Hii si tu kwa ajili ya mawakili hawa, bali mawakili wote nchini kuhakikisha wanazingatia sheria na kuwa waaminifu. Hii ni kwa sababu kuna tabia iliyoanza kuota mizizi ya mawakili kuruhusu watu kuwawakilisha kortini,” alisema.
“Hii ni hatari sana katika utoaji wa haki pale inapotokea amri imetolewa dhidi ya upande uliofika mahakamani ambao wala haufahamu nini kinaendelea,” alisema Jaji katika uamuzi wake huo ambao Mwananchi inayo nakala yake.
Jaji aliendelea kusema kuwa kilichofanywa katika shauri hilo si ni ukiukwaji wa maadili kwa upande wa mawakili, lakini ni jinai kutumia jina la mtu na kuwakumbusha mawakili hao kuhusu sheria inayosimamia ukiukwaji wa maadili.
“Makosa yanayokatazwa na sheria hiyo ndio yamefanywa katika maombi yaliyo mbele yangu. Nimechoshwa na hii tabia na sitaivumilia tena. Siwezi kukaa hapa mbele kutoa hukumu au uamuzi kwa kutumia nyaraka bandia,”alisema Jaji Matuma.
Kutokana na hicho alichokiona, alisema maombi hayo ya dhamana ni batili mbele ya macho ya sheria, kwani yalipelekwa mahakamani kwa kutumia nyaraka za kughushi.
Jaji Matuma alikielekeza Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Kanda ya Mwanza, kusambaza uamuzi wake huo kwa mawakili wengine katika mkoa huo, ili kuchukua tahadhari na akikutana na kituko kama hicho siku zijazo atachukua hatua.
Hatua hizo ni pamoja na za kisheria, ikiwamo kuwasimamisha uwakili na kupeleka suala lao kamati ya maadili ya mawakili, ili washughulikiwe kwa mujibu wa sheria na akataka wakili anayejua ana maombi ya aina hiyo ayaondoe mahakamani.