Kakolanya anavyojipanga Namungo | Mwanaspoti

KIPA mpya wa Namungo FC, Beno Kakolanya ametaja matarajio yake ya msimu ujao kuwa ni kuipambania timu kumaliza  nafasi nne za juu, ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Kakolanya amejiunga na Namungo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Ihefu ambako alisaini miaka miwili baada ya kuachana na Singida Fountain Gate.

Amesema, “matarajio ni kuona tunamaliza nafasi ambayo itatupa kushiriki michuano ya kimataifa itakayofanya tuzidi kuonyesha vipaji vyetu kwa ukubwa zaidi.”

Kitu kinachompa imani ya kufanya vizuri Kakolanya ni mastaa wazoefu walipo ndani ya kikosi hicho, anaoamini kwamba wana uwezo mkubwa wa timu hiyo kupata matokeo ya ushindi pindi Ligi Kuu itakapoanza.

“Ndani ya timu kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa na wazoefu mfano Meddie Kagere, Erasto Nyoni nimeona wanachofanya katika mazoezi kinachonipa picha ya kile ambacho watakifanya ligi itakapoanza,” amesema Kakolanya ambaye aliwahi kuzichezea Simba na Yanga zinazopata nafasi ya kucheza mara kwa mara michuano ya CAF.

Ametoa shukrani kwa mapokezi kutoka kwa wachezaji wenzake, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wa Namungo hivyo anaamini katika umoja huo watafanya mambo makubwa msimu ujao.

“Timu ikiwa na umoja ni silaha kubwa ya mafanikio. Ndio maana naiona Namungo kufanya vizuri na kumaliza nafasi za juu msimu ujao,” amesema.

Related Posts